Habari Mseto

Pendekezo jipya latolewa wabunge wapunguziwe mihula ya kuhudumu

Na JOSEPH OPENDA November 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BUNGE la kitaifa limepokea ombi jipya linalopendekeza kupunguzwa kwa muda wa kuhudumu kwa viongozi waliochaguliwa kuwa mihula miwili pekee; sawa na ya rais na magavana.

Ombi hilo, linalotarajiwa kuibua mjadala mkubwa nchini, limewasilishwa na kundi moja la kutetea haki za raia linaloendesha shughuli zake katika kaunti ya Nakuru.

Kulingana na kundi hilo, hatua hiyo inalenga kuweka usawa miongoni mwa wanasiasa na kutoa nafasi kwa wapiga kura kufaidi kutokana na talanta ambazo viongozi wengine wanazo.

Kundi hilo kwa jina “Grassroot Civilian Oversight Initiative” linapendekeza kuwa wabunge, maseneta na madiwani wawe wakihudumu kwa muda usiozidi mihula miwili (ya miaka miwili kila moja) sawa na marais na magavana, pamoja na manaibu wao.

Mshirikishi wa kundi hilo Laban Omusundi anawataka wabunge kupitisha ombi hilo ili kuhakikisha uwepo wa usawa katika uwakilishi.

Akirejelea vipengele vya 37 na 119 vya Katiba, Bw Omudundi anasema kuwa wataalamu walioandika Katiba waliweka mihula ya kuhudumu kwa rais na magavana kuwa miwili pekee kwa sababu nzuri, ambayo pia inafaa kutumiwa kwa nyadhifa nyingine za kisiasa.

“Viongozi wengine waliochaguliwa wanafaa kuhudumu kwa mihula miwili pekee ili kudumisha usawa na kuwezesha wananchi kufaidi kutokana na talanta za viongozi wengine ibuka,” akaeleza Bw Omusundi.

Alisema sio haki kwa tapo moja la viongozi kuhudumu kwa mihula miwili pekee ilhali wengine wanaruhusiwa kuhudumu milele.

Kulingana na Bw Omusundi, huku juhudi zikiendelezwa za kuboresha Kenya kwa manufaa ya raia wote, sheria zingine zinatoa nafasi kwa watu fulani kujifanya “wamiliki daima” wa nyadhifa zingine

Kulingana na kipengele cha 142 cha Katiba, mtu haruhusiwi kushikilia wadhifa wa urais kwa zaid ya mihula miwili ya miaka mitano kila moja.

Pendelezo la kundi la Grassroot Civilian Oversight Initiative linajiri wakati ambapo Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’wa amependekeza kuwa muda wa muhula wa viongozi waliochaguliwa upunguzwe kutoka miaka mitano hadi miaka minne.

Seneta huyo anasema muhula wa miaka minne utasaidia utachangia kuimarika kwa uwajibikaji huku ukitoa nafasi kwa watu wengi kushiriki katika shughuli za siasa.

Kulingana na Bw Thang’wa, pendekezo hilo linatoa nafasi kwa watu wengine kushikilia nyadhifa za uongozi na kuchangia katika utawala.

Seneta huyo wa Kiambu anaongeza kuwa muhula wa miaka minne pia utaimarisha misingi ya kidemokrasia nchini.

“Wakenya watapata nafasi zaidi ya kuhakikisha kuwa viongozi wanawajibika muhula wa uongozi ukiwa miaka minne pekee. Wapiga kura pia watapata muda wa kuhakiki utendakazi wa viongozi wao,” Bw Thang’wa akaeleza.

Seneta huyo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) anaongeza kuwa Wakenya watakuwa na hamu zaidi ya kushiriki uchaguzi ikiwa muhula wa viongozi kuhudumu utakuwa fupi.

Pendekezo la kufupisha muhula wa viongozi kuhudumu kutoka miaka mitano hadi minne limejiri baada ya Seneta wa Nandini Samson Cherargei kupendekeza kuwa muda wa muhula wa viongozi waliochaguliwa uongezwe kutoka miaka mitano hadi saba.

Pendekezo hilo limekataliwa na Kamati ya Seneti kuhusu Sheria na Masuala ya Kikatiba baada ya asilimia 99 ya Wakenya waliotoa maoni yao kulihusu kulipinga.