Habari Mseto

Pesa na simu husambaza maradhi – Utafiti

May 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ELIZABETH MERAB

WATAFITI wameonya kuhusu jinsi sarafu na simu za mkononi zinavyoeneza uchafu tele unaosababisha maradhi kwa binadamu.

Hela, haswa sarafu na noti za thamani ya chini; wanasayansi wanasema zinasababisha maradhi ya kuharisha miongoni mwa Wakenya wanaokula katika vibanda vya kuuza chakula.

Utafiti uliofanywa miongoni mwa wafanyabiashara wa vyakula kwenye hoteli 15 katika Kaunti ya Nairobi na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (Jkuat), Taasisi ya Utafiti wa Matibabu (Kemri) na Kitengo cha Utafiti wa Matibabu cha Jeshi la Amerika, unaonyesha kuwa fedha na simu huwa hazisafishwi hivyo hutumika kama maficho ya viini vinavyosababisha magonjwa.

Wanasayansi hao walipima sarafu zote kuanzia Sh1 hadi Sh1,000 zinazotumiwa jijini Nairobi. Watafiti walibaini kuwa sarafu ya Sh5, Sh10 na Sh20 ndizo chafu zaidi zikifuatiwa na noti ya Sh Sh50, Sh100 na Sh200.

“Hela hizo pamoja na simu zimesheheni viini vinavyosababisha kuhara na maradhi mengineyo,” unasema utafiti uliowasilishwa katika Kongamano la saba kuhusu Afya na Sayansi Afrika Mashariki lililofanyika jijini Dar es Salaam, Tanzania mnamo Machi, mwaka huu.

Jambo la kutisha zaidi ni kwamba waandaaji wa chakula kama vile wapishi na wahudumu, hawazingatii usafi kwani wanatumia simu na kushika fedha bila kunawa hivyo kusambaza maradhi zaidi.

Waandaaji wa chakula 34 waliokuwa miongoni mwa watu waliofanyiwa utafiti walikuwa wagonjwa walikuwa wakiugua kikohozi, nimonia na kuwashwa na tumbo.

Maradhi hayo husambaa kutoka kwa wahudumu wagonjwa hadi kwa walaji.

Watafiti hao walibaini kuwa asilimia 60 ya wahudumu hawasafishi mikono baada ya kutumia simu au kushika fedha.

Kwa kawaida, hela zinafaa kushughulikiwa na watu tofauti na wahudumu.

“Wauzaji wa chakula na Wakenya kwa ujumla wanastahili kuelimishwa kuhusu athari za kushika simu, hela pamoja na chakula,” wanaonya watafiti hao. Mnamo 2009, taasisi ya Kemri ilifanya utafiti sawa jijini Nairobi na kubaini kuwa hela zimesheheni viini vinavyopatikana katika kinyesi.

Nyingi ya fedha zilizokuwa na viini vingi ni sarafu za bucha za kuuza nyama na vibanda vya kuchoma mahindi.

Kulingana na Dkt Richard Korir, mtafiti katika taasisi ya Kemri na mmoja wa wanasayansi walioendesha utafiti huo, maradhi ya kuhara yanachangiwa na waandaaji wa chakula wanaotumia simu na kushika simu bila kuosha mikono.

Utafiti ulibaini kuwa viini vinavyopatikana katika hela au simu vinasababisha homa ya matumbo, kichocho, kipindupindu na hata maradhi ya ngozi.

“Noti ya Sh1,000 ina kiasi kidogo cha viini kwa sababu haitumiki kwa wingi ikilinganishwa na sarafu na noti za thamani ya chini,” akasema Dkt Korir.

Kiini kilichopatikana katika hela zote ni staphylococcus ambacho husababisha maambukizi ya maradhi ya ngozi, moyo, nimonia na kusababisha sumu katika chakula.

Viini vingine vilivyopatikana ni aina ya Bacillus ambavyo husababisha chakula kuwa na sumu, homa ya uti wa mgongo, mshtuko na kuathiri damu.