Pesa nilizoweka kwa nyumba nitanunua 'mathwiti na makeki'- Kuria
Na PETER MBURU
MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria sasa ameanza kuwakejeli watu anaosema walikuwa wamehifadhi mabunda ya pesa nyumbani mwao, akisema huenda wakapata hasara kubwa.
Akitumia lugha ya utani alipokuwa akihutubia waumini katika kanisa moja, Bw Kuria alisema kufikia Oktoba, wale ambao hawatakuwa wametumia pesa hizo huenda wakalazimika kuzitumia kama malazi kwa mifugo, kwa kuwa hazitakuwa na kazi.
“Mtu aliye na pesa zake ndani ya nyumba tulipewa miezi minne tutoe zote. Msipozitumia katika muda huo mtajipanga. Sasa noti za Sh1,000 zitakuwa zikitumiwa kuunda malazi ya ngombe kuanzia Oktoba,” Bw Kuria akasema.
Akimpongeza Rais Uhuru Kenyatta na Gavana wa Benki Kuu Patrick Njoroge, mbunge huyo alisema “Rais alifanya vizuri kwa kuwa ufisadi unaelekea kumaliza hili taifa.”
Lakini alisema pia naye hajaachwa nyuma kufuatia agizo hilo kwani pia ana pesa, lakini akasema zake atazitumia kununua “mathwiti na makeki” kabla ya muda huo kukamilika.
“Mimi zangu nitaenda nikinunua ‘mathwiti na makeki’ hadi ziishe. Tutumie huu wakati, kwa kuwa ukienda huko (kuzibadilisha) utaulizwa hizi ulitoa wapi na ulikuwa umeweka wapi,” Bw Kuria akasema.
Mbunge huyo pia aliwapuuza viongozi wa mirengo ya ‘Tangatanga’ na ‘Kieleweke’ akisema hawana maana na kuwa atawabwaga.
“Niliwaambia turudi nyuma ya hema. Hawa wanajiita Tangatanga na Kieleweke nitawagonga wote ni mimi tu nitasalia kuvuma huku peke yangu,” akasema.