Pigo kwa Kenya baada ya China 'kukataa' kuipa mkopo wa Sh380bn kuendeleza SGR Naivasha hadi Kisumu
Na CHARLES WASONGA
NI pigo kuu kwa serikali ya Kenya baada ya China kuinyima mkopo wa Sh380 bilioni za kufadhili ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Kisumu.
Hii ni baada ya ujumbe wa Kenya ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kufeli kuelewana na Serikali ya China kuhusu masharti ya mkopo huo.
Duru zasema kuwa serikali ya Kenya ilitaka mkopo wa riba ya chini na isiyowekewa mali ya serikali kama dhamana lakini China ikakataa.
Serikali ya Rais Xi Jinping ilisema inaweza kugharamia ukarabati wa reli ya zamani (meter gauge line) kwa gharama ya Sh40 bilioni.
Akiongea na wanahabari Ijumaa, Waziri wa Uchukuzi na Miundombinu James Macharia alisema serikali itaelekeza juhudi zake katika ukarabati wa reli ya zamani kutoka Naivasha hadi Kisumu na hatimaye Malaba ili kufanikisha usafirishaji wa bidhaa kutoka Bandari Kavu ya Naivasha hadi magharibu mwa Kenya na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.
“Huku serikali ikiendelea na mazungumzo kuhusu masharti mazuri ya mkopo kuwa kujenga awamu ya 2B ya SGR kutoka Naivasha hadi Kisumu, serikali itarekebisha reli ya zamani ili kurahisisha usafiri wa bidhaa kutoka Naivasha hadi magharibi mwa Kenya,” akasema Waziri Macharia.
Wakati uo huo, Bw Macharia alisema mfumo wa uchukuzi kutumia mabasi ya kubeba abiria wengi uliosubiriwa kwa hamu kuu sasa utazinduliwa Juni 2019.
Mabasi mawili ya kwanza yanatarajiwa kuwasili nchini mwezi ujao wa Mei kutoka Afrika Kusini.