Habari Mseto

Polisi kulipwa kulingana na uhalali wa vyeti vyao

March 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na NDUNGU GACHANE

WIZARA ya Usalama itatumia mfumo wa kidijitali katika idara yake ya wafanyakazi ya Huduma za Polisi kuhakikisha maafisa wa polisi wanatambuliwa na kulipwa kulingana na kiwango cha elimu yao.

Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i alisema polisi pia watalipwa kulingana na uhalali wa stakabadhi walizowasilisha.

Waziri alisema hayo katika kituo cha polisi cha Githumu, eneo la Kandara, Kaunti ya Muranga kufuatia ripoti kuwa polisi wanatisha kujiuzulu kwa wingi kwa sababu ya uamuzi wa kupunguza mishahara yao. Hata hivyo, uamuzi huo umebatilishwa.

Alieleza kuwa kwa kufanya ukaguzi wa kina na kutumia mifumo hiyo ya kidijitali, wizara itaweza kujua inaowalipa pamoja na viwango.

“Kufikia mwaka ujao wa fedha baada ya kuweka mifumo ya kidijitali kwa idara ya wafanyakazi ya Huduma za Polisi, tutaweza kuwa na maelezo ya kila mtu na jinsi tunavyowalipa. Hii haitajumuisha polisi pekee bali pia machifu na wasaidizi wao na maafisa wengine katika utawala,” alisema.

Aliongeza, “Hatutavumilia biashara hii ambayo imekuwa ikiendelea katika idara ya Wafanyakazi na tutasafisha na kuangalia mishahara ya polisi,” alisema Dkt Matiang’i.

Alishtumu Huduma ya Polisi ya Kitaifa kwa “kuamka asubuhi na kuwashangaza polisi na mishahara mipya.”| Wakati huo huo, waziri aliwataka polisi kuelekeza malalamishi yao kupitia njia zinazostahili na sio kuzitoa nje ya kikosi.

“Nataka kuwakumbusha polisi kuwa wao ni kitengo cha usalama na hawafai kupeleka masuala yao ya ndani kwa Facebook kwa kufanya hivyo ni kuingiza siasa kwa mashauri ya polisi,” alionya.