Polisi sasa kuanza kupiga mnada pikipiki na tuktuk zilizokwama vituoni
WAMILIKI wa pikipiki, tuk tuk na magari yanayozuiliwa katika vituo vya polisi vya Kadzandani na Nyali, Kaunti ya Mombasa, wamepewa siku saba kuyachukua la sivyo yapigwe mnada.
Matangazo yaliyochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali Ijumaa iliyopita yalisema kibali cha kupiga mnada mali hizo kilishatolewa na Mahakama ya Shanzu.
Kulingana na matangazo hayo, mali hizo zitauzwa na kampuni ya upigaji mnada kwa niaba ya vituo vya polisi, kwa msingi wa sheria za Kenya.
Shughuli sawa na hii imepangwa pia kufanyika katika kituo cha polisi cha Ruiru, Kaunti ya Kiambu, ambapo wamiliki wa magari na pikipiki wametakiwa kuyachukua kabla ya siku 30 kukamilika.
Mali nyingine zitakazouzwa na kampuni ya upigaji mnada kwa niaba ya kituo hicho ni vyuma, mbao, plastiki na baisikeli.
Wakati huo huo, wakazi wa Kisiwa cha Mkwiro kilicho Lungalunga, Kaunti ya Kwale, wameitaka serikali ya kaunti kujenga kuta za kukinga bahari ili kuwalinda dhidi ya kuathiriwa na viwango vya maji ya bahari vinavyoendelea kupanda.
Wakazi hao walisema tayari baadhi ya maeneo yameanza kuingiliwa na maji ya bahari kutokana na mafuriko na mmomonyoko wa udongo, hali ambayo imesababisha uharibifu.
Kuta za bahari hujengwa kati ya ardhi na maji ili kuzuia maji kutoka baharini kuingia kwenye maeneo ya makazi, lakini sehemu kadha za ufuoni Kaunti ya Kwale hazina kuta hizo.
“Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumeona maji ya bahari yakiendelea kusogea kuelekea nchi kavu,” akasema Bw Mshemanga Hamisi, mwanachama wa kikundi cha Pongwe Kidimu Community Forest Association.
Akizungumza akiwa Diani, Bw Hamisi alisema wakazi wana wasiwasi kuwa athari zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi zitasababisha mafuriko ya maji katika makazi yao.
Katika mahojiano ya awali, Mkurugenzi wa Idara ya Hali ya Hewa ya Kenya, Dkt David Gikungu, aliwashauri wakazi kupanga kuhamia maeneo ya juu zaidi kwa kuwa viwango vya maji vinatarajiwa kuongezeka zaidi.
Hii ni baada ya mnamo mwezi Aprili mwaka huu, ambapo maji ya bahari yalipanda ghafla na kufika vijijini katika maeneo kadha ya Wasini na Vanga katika Kaunti ya Kwale.