54%: Polisi waliongoza kwa ubakaji uchaguzi mkuu wa 2017 – KNCHR
Na PETER MBURU
MAAFISA wa usalama nchini walikuwa mstari wa mbele kutekeleza unyama wa dhuluma za kingono wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, Tume ya Kitaifa Kuhusu Haki za Binadamu (KNCHR) imesema.
Tume hiyo ilisema kuwa kati ya visa 201 vya ubakaji, unajisi na ubakaji wa magenge ambavyo ilipokea kutoka Agosti 11 baada ya matokeo ya uchaguzi wa Urais kutangazwa, asilimia 54.5 ya wadhulumiwa walidai kutendewa unyama huo na polisi.
KNCHR ilisema hivyo Jumatano wakati ilipozindua ripoti kuhusu dhuluma za kingono wakati na baada ya uchaguzi huo wa mwaka jana, ripoti ambayo imelaumu vikubwa serikali na kulitaka bunge kurekebisha sheria kuhusu dhuluma za kingono ili kuwasaidia wanaodhulumiwa.
Tume hiyo aidha imemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuomba msamaha wa umma kutokana na ukatili ulioendelezwa na maafisa wa serikali, ikisisitiza kuwa visa hivyo vilijirudia kutoka uchaguzi uliopita na hivyo kuna hatari kuwa vitajirudia siku za usoni.
“Kwa hawa Wakenya ambao walijitokeza kupiga kura ili kutimiza wajibu wao wa kikatiba lakini wakakumbana na ukatili huu ambao tumeunakili, Rais aombe msamaha mbele ya umma akisema kuwa serikali yake inapinga visa vya dhuluma za ngono,” naibu mwenyekiti wa tume hiyo George Morara akasema.
Mwenyekiti wa tume hiyo Bi Kagwiria Mbogori alishauri asasi mbalimbali za serikali kuchukulia ripoti hiyo kwa uzito na kutatua palipokosolewa, ili taifa liepuke visa hivyo tena katika chaguzi za mbele.
“Inatarajiwa kuwa wakati wa fujo, asasi za usalama zinafaa kuongoza kulinda raia na kuwakamata wanaochochea ghasia. Hali ambapo zinageuka na kuwa maafisa wake wanaongoza kudhulumu watu kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa 2007-2008 na kurudiwa katika uchaguzi wa 2017 ni sababu ya kuwashtua Wakenya wote,” Bi Mbogori akasema.
Utafiti wa tume hiyo ulijikita katika kaunti tisa ambazo ziliadhirika zaidi, zikiongozwa na Nairobi, Kisumu, Vihiga, Kakamega, Migori, Siaya, Busia, Homa Bay na Bungoma.
Kati ya watu 201 walioripoti kudhulumiwa, asilimia 96.26 walikuwa wanawake, asilimia 3.74 wakiwa wanaume. Kiumri, mwanamke zaidi aliyedhulumiwa alikuwa na miaka 70 na mwanaume 68, huku mtoto mchanga zaidi aliyenajisiwa akiwa na miaka saba.
“Kwa baadhi ya watoto ambao hawakudhulumiwa kimwili, walilazimika kutazama wakati wazazi wao walikuwa wakibakwa, visa vyenye uzito ambao hawangeweza kuhimili,” ripoti hiyo imesema.
Tume hiyo ilieleza wasiwasi wake kuwa japo ina uhakika kuwa visa vingi zaidi vya dhuluma hizo vilitendeka, watu wengi walisalia kimya kwa hofu za kuadhiriwa na waliowatendea unyama. Baadhi ya vituo vya polisi vimedaiwa kudinda kunakili malalamishi ya wadhulumiwa viliposikia kuwa ni maafisa wa polisi waliotekeleza unyama.
“Dhuluma za ngono ni mojawapo ya uvunjaji wa haki za binadamu kwa viwango vikubwa zaidi na hakuna Mkenya anafaa kutendewa hivyo kwa sababu tu ya tofauti za kisiasa,” ripoti ya KNCHR imeshauri.
KNCHR sasa inalitaka bunge kufanyia marekebisho sheria kuhusu dhuluma za kingono na kulainisha baadhi ya masuala ambayo yamezuia haki kupatikana.
Bw Morara alisema kuwa ilivyo kwa sasa, sheria hiyo inahitaji mdhulumiwa wa unyama huo kudhihirisha kwa viwango vya juu zaidi ili mshukiwa kuadhibiwa, jambo alilosema kuwa limefanya vigumu kwa tume hiyo kufanikiwa katika kesi inazowasilisha kortini.
“Dhuluma za ngono baada ya uchaguzi ilikuwa mbinu moja ya ghasia ambayo haikuzungumziwa licha ya kuadhiri Kenya kufuatia uchaguzi wa 2007 na inaweza kujirudia endapo haitaangaziwa,” ripoti ya KNCHR ilirejelea maneno haya kutoka kwa ripoti ya Jaji Philip Waki kuhusu fujo zilizozuka baada ya uchaguzi wa 2007/08.