Habari Mseto

Polisi wanyakwa wakimeza hongo

November 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAUREEN ONGALA

MAAFISA wawili wa polisi walitiwa mbaroni wikendi walipofumaniwa na Kamanda wa polisi eneo la Pwani, Bw Rashid Yaqub, kwa madai ya kuchukua hongo.

Maafisa hao wa kituo cha polisi cha Kilifi walinaswa katika eneo la Mavueni katika barabara kuu ya Mombasa –Malindi mwendo was saa moja asubuhi.

Bw Yaqub alisema alikuwa anatoka Malindi kutoka Mombasa wakati aliona manamba wa matatu ikiangusha kitu kwa maafisa hao wa polisi.

“Nilisimamisha gari langu na kisha nikaokota kile manamba yule alikuwa ameangusha na kugundua kuwa ilikuwa na ni noti ya shilingi mia moja,” akasema.

Yaqub aliokota pesa hiyo na akawaamuru maafisa hao kupanda garini mwake kisha akawapeleka katika kituo cha polisi cha Kilifi.Aliwakabidhi kwa Kamanda wa polisi anayesimamia eneo bunge la Kilifi Kaskazini Njoroge Ngigi na kuamuru watiwe korokoroni.

Maafisa hao Inspekta Joseph Kirui na Koplo Patrick Safari, waliachiliwa kwa bondi ya polisi ya Sh3,000 kila mmoja.Kamanda huyo wa eno la Pwani alisema kuwa maafisa hao watachukuliwa hatua za sheria za kindani kulingana na kikosi cha polisi.

“Tutashughulikia swala hilo kindani lakini tusipofanikiwa tutawafikisha mahakamami,” akasema Bw Yaqub.Alisema kuwa maafisa hao hawatakabidhiwa maafisa wa EACC.

Maafisa hao walikataa kuongea na wanahabari.“Hatuna mamlaka ya kuongea na wanahabari. Tafadhali tafuteni habari kwa mkubwa wetu.

Tulikabidhiwa kwake na tumenakili kila kitukilichotukia,” wakasema.Hata hivyo mmoja wa afisa wakuu katika kituo cha polisi cha Kilifi, alisema itakuwa vigumu kuwashtaki wawili hao kwani ni haijabainika iwapo mkubwa huyo wa polisi alikuwa amewawekea mtego au la.