Habari Mseto

Polo akataa kuketi baada ya kutahiriwa

August 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY WAWERU

Eworet, Bomet

KIJANA mmoja aliyepashwa tohara katika kijiji hiki alikataa kuketi chini akitaka babake mzazi kutimiza ahadi ya kumpa zawadi ya ng’ombe.

Inasemekana baba yake aliahidi kumpa ng’ombe iwapo angestahimili kisu cha ngariba. “Mimi nikiwa babako nitakupa ng’ombe kama utafaulu kwenye tohara,’’ mzee alimuahidi.

Kulingana na mdokezi, babake alikuwa na wasiwasi huenda mwanawe angepiga nduru mbele ya umati kijijini wakati wa kupashwa tohara. Hii ilimfanya amuahidi ng’ombe kumtia motisha afaulu ‘mtihani’ huo.

Siku ya tohara, boma lote lilikuwa limejaa watu, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo. Wazazi wa kijana walikuwa na wasiwasi. Hata hivyo, kijana huyo alisimama tisti na kutahiriwa.

Sekunde chache baadaye, firimbi ililia kuashiria kwamba alikuwa amefaulu mtihani. Babake hakuamini kwamba mwanawe alikuwa amekuwa mtu mzima.

Kulingana na mdokezi, kijana alimfunika leso na kutakiwa kuketi lakini alikataa katakata kufanya hivyo. Alisema alikuwa akitaka zawadi yake. Watu walishtuka kumuona kijana akikataa kuketi kwenye kiti hadi baba yake atimize ahadi.

Ilibidi baba yake aitwe kudhibitisha iwapo alitoa ahadi hiyo au la. “Baba yake alikubali. Aliagiza ng’ombe mmoja kuletwa na kukabidhiwa kijana.

Alisema kijana alikuwa na haki ya kidai zawadi aliyomuahidi kwa sababu alikuwa ameonyesha ni mwanamume kamili,” alisema mdokezi.

Vigelegele, shangwe na nderemo zilitanda huku wakazi wakifurahia vyakula na pombe ya busaa kwa wingi.

Kulingana na mila na desturi za jamii ya eneo hili, kijana anayepashwa tohara huwa na haki ya kuitisha chochote anachotaka kabla ya kuketi au kuingizwa kwenye nyumba.