Habari Mseto

Raia wa Amerika asukumwa jela kwa ulaghai wa Sh46 milioni

Na RICHARD MUNGUTI March 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIA wa Amerika amesukumwa kizuizini akisubiri kushtakiwa kwa ulaghai wa Dola za Amerika 357,300 (Sh46 milioni).

Philip William Knight aliyeamriwa ashtakiwe Machi 27, 2025 anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol, Nairobi.

Knight alifikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani kufuatia malalamishi na Bw Casey Drew Cain katika kituo hicho cha Capitol Hill kwamba alitapeliwa Sh46 milioni akielezwa mamilioni hayo ni ya kuwekeza katika biashara ya dhahabu, kutoa mafunzo kwa kina mama na kusambaza chakula katika kambi za wakimbizi Kakuma kupitia World Food Programme (WFP).

Akitoa uamuzi katika ombi lililowasilishwa na maafisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) la kumzuilia Knight kwa siku 10, hakimu alisema mshukiwa huyo ameoa Mkenya, Amina Mohammed na wamejaaliwa watoto watatu.

Hakimu alitupilia mbali ombi la kumzuilia kwa siku 10 Knight akisema “hakuna sababu za kutosha zilizowasilishwa na mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kupitia kwa wakili wa serikali Joyce Olajo.”

Akiomba mshukiwa huyo wa ulaghai asukumwe kizuizini kwa siku 10, Bi Olajo alisema Knight atatoroka kwa vile hana makazi Nairobi.

Pia, alidai polisi wanamsubiri mlalamishi mwingine Dkt William B Woodmark kusafiri kutoka Amerika kuandikisha taarifa.

Hali kadhalika, wakili wa serikali alidai maafisa wa DCI walikuwa wanasubiri kupokea rekodi ya Benki ya Wells Fargo ya Amerika ambapo Dkt Woodmark alimtumia Knight Dola za Amerika 281, 000 kufadhili mradi wa chakula wa WFP.

Mahakama pia ilielezwa Knight alikuwa ameahidi Cain kwamba mradi huo wa WFP utawapa faida ya Dola za Amerika 125 milioni (Sh16 bilioni).

Ili kufanikisha mradi huo, mahakama ilielezwa mshukiwa alimtaka awekeze pesa hizo kupitia kwa makampuni yake Sunshine Minerals Canada Limited (SMCL) na Hallo Global Project Management Limited.

Mshukiwa huyo hata alimteua Bw Cain kuwa Meneja wa mradi huo wa usambazaji chakula wa WFP.

Katika uamuzi wake, Jaji Lucas Onyina alisema polisi wanaweza kupata rekodi ya benki kwa njia ya mtandao na kwamba mahakama haitakiuka haki za mshukiwa ikimsubiri Dkt Woodmark kutoka Amerika kufika kuandikisha taarifa.

Mahakama iliamuru mshukiwa azuiliwe kwa siku moja kisha alipe dhamana ya Sh1 milioni ifikapo Machi 27, 2025 atoke kituo cha polisi cha Capitol Hill.

Knight alitiwa nguvuni Machi 22, 2025 akirejea nchini kutoka Amerika.