Habari Mseto

Rais aahidi kutekeleza mapendekezo ya sukari

February 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ameahidi kuwa serikali itatekeleza mapendekezo ya jopokazi kuhusu sukari kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za kufufua sekta hiyo.

Rais alitoa hakikisho hilo jana katika Ikulu ya Nairobi alipopokea ripoti ya jopokazi hilo ambalo aliliteua kuangazia sekta hiyo ya sukari.

Rais Kenyatta aliliambia jopokazi hilo linaloongozwa na Waziri wa Kilimo Peter Munya, pamoja na Gavana wa Kaunti ya Kakamega Wycliffe Oparanya, kwamba serikali iko makini kuhakikisha wakulima wa miwa nchini wananufaika kutokana na kilimo chao.

Mapendekezo makuu ya ripoti hiyo ni kuanzishwa tena kwa ushuru wa sukari, kubinafsishwa kwa viwanda vya umma ili kuboresha utendakazi pamoja na kubuniwa kwa sheria kuhusu sukari.

Ushuru huo wa sukari utatozwa watumiaji ili kuwe na pato linalohitajika kuwasaidia wakulima.

Mapendekezo mengine ambayo yamewasilishwa ni pamoja na kuchapishwa kwa kanuni za sekta ya sukari katika gazeti rasmi la serikali ikiwemo kuhusu uagizaji sukari kutoka mataifa ya kigeni, na kubadilishwa kwa utaratibu wa kutoza ushuru katika sekta hiyo ili kuboresha marupurupu kwa wawekezaji.

Jopokazi hilo pia limependekeza kwamba kanuni za shirika la COMESA zitekelezwe kikamilifu.

Kuhusu ubinafsishaji, Rais Kenyatta aliyeandamana na Naibu Rais William Ruto, alisema serikali haihitaji kuhusika katika biashara ya sukari kwa sababu wajibu wake ni kuwasaidia wakulima kupata mbegu bora, mbolea ifaayo na pembejeo muhimu za kilimo.

“Sekta ya kibinafsi itafanya biashara huku wajibu wetu ukiwa kufanikisha masilahi ya wakulima. Tutafute njia bora zaidi za kutimiza hili,” akasema.

Rais alilishukuru jopokazi hilo ambalo lilibuniwa Novemba 2018 kwa kukamilisha wajibu huo kwa wakati ufaao, na kulitaka lidumu hadi mchakato wote wa kufufua sekta hiyo utakapokamilika.

Gavana Oparanya alisema jopokazi hilo limeridhika kwamba kwa kutekeleza ripoti yao, taifa litaweza kufufua viwanda vyake vinavyokabiliwa na matatizo, na hivyo kunufaisha mamilioni ya wakulima.

Mawaziri Peter Munya wa Kilimo na Ukur Yattani wa Hazina Kuu pamoja na Magavana Prof Anyang Nyong’o wa Kisumu na Wycliffe Wangamati wa Bungoma ambao ni wanachama wa jopokazi hilo pia walihudhuria mkutano huo.