Habari Mseto

Rais aelekea Uingereza kutafuta ufadhili

January 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na AGGREY MUTAMBO

RAIS Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzuru jijini London, Uingereza, kuanzia leo Jumapili kuanza juhudi za kutafuta ufadhili zaidi wa miradi mbalimbali iliyo chini ya Ajenda Nne Kuu za Maendeleo.

Ziara yake ni sehemu ya mwaliko aliopata kuhudhuria Kongamano la Uwekezaji kati ya Uingereza na Afrika linaloanza Jumatatu.

Rais anatarajiwa kuwatafuta wawekezaji zaidi kumsaidia katika masuala ya utengenezaji bidhaa, ujenzi wa nyumba, uboreshaji wa sekta ya afya na kilimo.

Masuala hayo ni miongoni mwa mipango mikuu iliyojumuishwa kwenye ajenda kuu za Rais Kenyatta.

Maafisa mbalimbali wa serikali waliiambia ‘Taifa Jumapili’ kwamba Rais ataangazia masuala ya kiuchumi, kinyume na ziara za awali, ambapo amekuwa akijikita katika masuala ya usalama na siasa za kikanda.

“Tunatarajia uwepo wa mashauriano ya kina kati ya wafanyabiashara wa Kenya na Uingereza kuhusu sekta zinazohitaji uwekezaji mkubwa. Vilevile, tunatarajia kwamba kutakuwa na mashauriano kati ya serikali za nchi hizo mbili kuhusu sekta ambazo Uingereza itaisaidia Kenya kiuchumi,” akasema Bw Manoah Esipisu, balozi wa Kenya nchini Uingereza.

Akaongeza: “Kenya imekuwa ikishinikiza masuala ya biashara na uwekezaji. Tunatarajia kuwa mazungumzo kuhusu masuala hayo kati ya mengine yatakuwa muhimu kwa ustawi wa raia wa Kenya na Uingereza.”

Rais Kenyatta ataandamana na maafisa kadhaa wa serikali, baadhi yao wakiwa Waziri wa Fedha Ukur Yatani, Waziri wa Mashauri ya Kigeni anayeondoka Dkt Monicah Juma na Gavana wa Benki Kuu ya Kenya (CBK), Dkt Patrick Njoroge.

Watatu hao wanatarajiwa kuwahutubia wawekezaji kuhusu hali ya uchumi nchini.

Katibu katika Wizara ya Ujenzi, Bw Charles Hinga na mwenzake wa Wizara ya Mafuta, Bw Andrew Kamau pia wanaenda. Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Wawekezaji Kenya (KPSA), Bi Carole Kariuki, mwenyekiti wake, Bw Nicholas Nesbitt na Mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara Kenya (KNCCI), Bw Richard Ngatia wataongoza wafanyabiashara.

Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Centum, Bw James Mworia na Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Equity, Dkt James Mwangi tayari wako London.