Habari MsetoKimataifaSiasa

Ruto anavyomuiga Trump kukabili mahasidi Twitter

September 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JEREMIAH KIPLANG’AT

NAIBU Rais William Ruto ameonekana kukumbatia mtandao wa Twitter katika siku za hivi karibuni kila anapotaka kukanusha taarifa zozote zinazoonekana kumharibia jina, hasa kutoka kwa vyombo vya habari.

Mkakati wake umefasiriwa kuiga ule wa Rais Donald Trump wa Amerika, ambaye amekuwa akitumia mtandao huo kuwakabili watu anaowachukulia kuwa mahasimu wake kisiasa ama vyombo vya habari vinavyoandika taarifa zinazomkasirisha.

Mnamo Jumapili mwendo wa saa tano usiku, Dkt Ruto alitumia akaunti yake ya Twitter kukanusha habari zilizoangaziwa na gazeti moja nchini kumhusu.

Kwenye ujumbe alioandika, Dkt Ruto aliweka picha yenye kichwa cha habari kuu za gazeti hilo, zilizohusu madai kwamba Rais Uhuru Kenyatta alimkwepa katika Uwanja wa Kitaifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) aliporejea nchini kutoka Japan mnamo Alhamisi iliyopita.

“Chama cha Jubilee kimejengwa kwa msingi thabiti hivi kwamba, hakuna njama zozote ama propaganda zitakazokisambaratisha,” ukaeleza ujumbe huo.

Ilikuwa ni mara ya pili chini ya wiki moja kwa Dkt Ruto kutumia mtandao huo kupuuzilia habari zilizochapishwa na vyombo vya habari kumhusu. Ana ufuasi wa watu 2.3 milioni kwenye mtandao huo.

Mwezi uliopita, alipuuzilia mbali habari kuu za gazeti lingine kuwa washirika wake wa kisiasa walikuwa wakipanga kupinga kura ya maoni kuhusu mageuzi ya kikatiba inayotarajiwa kupendekezwa na Jopo la Maridhiano (BBI) lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Kabla ya kuanza kutumia mitandao ya kijamii, Dkt Ruto alikuwa akipuuzilia mbali baadhi ya habari zinazomhusu, ambapo mara nyingi aliwategemea washirika wake kuzikanusha.

Katika nyakati zingine, alikuwa akikanusha habari hizo kwenye mikutano ya umma.

Kwa sasa, mtandao huo unaonekana kuwa jukwaa lake analopendelea zaidi.

Jana, Msimamizi Mkuu wa Mawasiliano katika afisi ya Naibu Rais, Bw David Mugonyi alisema Dkt Ruto anaamini katika uhuru wa vyombo vya habari, ambapo ndipo ameamua kuvituamia ili kujielezea.

“Naibu Rais anaamini katika uwepo wa vyombo vya habari. Hilo linajumuisha haki ya kufanya makosa, lakini si kubuni habari za uongo kwa malengo ya kisiasa. Hiyo ndiyo sababu kuu ambapo bado hajavishtaki vyombo hivyo, licha ya kuwa na haki ya kisheria kufanya hivyo. Badala yake, amechagua njia ya kueleza ukweli kupitia mitandao ya kijamii,” akasema Bw Mugonyi.

Hata hivyo, Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa Bazara la Vyombo vya Habari Kenya (MCK) Bw Victor Bwire alisema kuwa Dkt Ruto anapaswa kutumia mkondo wa kisheria kueleza matatizo yoyote dhidi ya vyombo vya habari.

“Naibu Rais ana haki ya kueleza tatizo lolote alilo nalo dhidi ya vyombo vya habari. Ni haki yake kufanya hivyo. Tungependa kumshauri atumie taratibu za kisheria. Tuko tayari kutathmini uhalali wa malalamishi yake,” akasema Bw Bwire, kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Mnamo Jumatatu, Bw Trump alivikashifu vikali vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikiandika taarifa za kumharibia jina.

Rais huyo ametoa matamshi ya kudhalilisha waandishi hasa katika kipindi hiki nchi hiyo inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao.