Ruto aondoke ifikapo 2022, Maina Kamanda amuunga mkono Murathe
SAMWEL OWINO, ONYANGO K’ONYANGO na WYCLIFF KIPSANG
MBUNGE Maalum Maina Kamanda amejitokeza kutetea naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe kutokana na matamshi yake ya juzi kuwa eneo la Mlima Kenya halina deni la kisiasa kwa naibu wa Rais William Ruto kwenye uchaguzi wa Urais wa 2022.
Bw Kamanda Ijumaa alieleza Taifa Leo kuwa Bw Murathe alizungumza kuwakilisha watu wengi ambao wako kimya katika chama hicho na hivyo hafai kukashifiwa kwa kusema ukweli.
“Wakati ukifika, tutarejelea maneno ambayo Bw Murathe amesema lakini kwa sasa tushughulike na kuunganisha taifa tu. Wale wanaomkashifu Bw Murathe waache kwani kile alichosema ndicho wanachama wengi wa Jubilee wanasema kichinichini ukizungumza nao,” akasema Bw Kamanda.
Mbunge huyo wa zamani wa Starehe alimtetea Bw Murathe wazi kuhusiana na matamshi yake ya Jumatano wakati wa kuadhimisha sherehe za 39 katika kabila la Maragoli.
Bw Murathe alisema eneo la Mlima Kenya halikuweka mkataba wa maelewano na mtu yeyote kuhusu chaguzi za Urais.
“Ikiwa ana mkataba na Rais Uhuru Kenyatta basi hayo yalikuwa makubaliano baina yao wawili,” akasema Bw Murathe katika kaunti ya Vihiga.
Matamshi yake tangu wakati huo yamekuwa yakiibua hisia kali kutoka kwa wandani wa Dkt Ruto ambao wamemlaumu kuwa anatoa “matamshi yasiyofaa licha ya kuwa afisa mkuu wa chama.”
Bw Kamanda alisema kuwa kujaribu kumnyamazisha Bw Murathe ni sawa na kuziba kidonda ambacho tayari kimetokota.
“Ukijaribu kuficha kidonda, siku moja kitaonekana na huenda wakati huo hakitaweza kutibika,” akasema.
Mbunge huyu alisifu ushirikiano wa Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwa umeleta amani nchini.
Kwingineko, wazee kutoka eneo la Bonde la Ufa walionya wanasiasa kujizuia kutoa maneno kutenganisha taifa kuhusiana na matamshi ya Bw Murathe, wakisema hayatasaidia hali.