• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:00 PM
Ruto awaonya Wachina wakora wanaovunja sheria Kenya

Ruto awaonya Wachina wakora wanaovunja sheria Kenya

CAROLYNE AGOSA NA DPPS

NAIBU Rais Dkt William Ruto ameonya raia wa Uchina humu nchini kuwa ni lazima wafuate sheria za Kenya ili kuendeleza uhusiano mwema baina ya mataifa hayo mawili.

Aidha, Dkt Ruto aliwataka Wachina kusita kujiingiza katika biashara na kazi zinazoweza kufanywa na Wakenya ili kujipatia riziki ya kila siku.

“Kenya inaongozwa na utawala wa sheria. Kwa hivyo, tunatarajia raia wa China kufuata sheria hizo, na pasipo na ufahamu watafute mwongozo kutoka kwa mamlaka simamizi,” alisema Dkt Ruto.

Naibu Rais alisema hayo ofisini mwake Karen alipotembelewa na Balozi wa Kenya humu nchini Bw Wu Peng.

Kumekuwa na visa vingi vinavyohusu Wachina wanaokiuka sheria ikiwemo mapema wiki hii ambapo Wachina wanne walikamatwa kwa kumpiga mhandisi wa Mamlaka ya Bararara Kuu za Kitaifa (KeNHA) katika Kaunti ya Turkana.

Bw Peng aliunga mkono onyo la Naibu Rais na kusema kuwa China imekerwa na visa vya raia wake kuonyesha mienendo isiyofaa.

Alisisitiza kuwa Wachina watakaovunja sheria wataadhibiwa vikali sio tu na Kenya bali pia “kupitia utaratibu wa ndani tulioweka kama China”.

“Raia wetu lazima watii sheria za Kenya. Wanafaa kufuata utaratibu sawa katika kupata vibali na leseni zinazohitajika,” akasema Balozi Peng na kuonya kuwa hataruhusu watu wachache kutia doa uhusiano mzuri baina ya Kenya na China.

“Iwapo Wakenya wana shaka kuhusu raia wa China, tuarifu. Lazima tufuate sheria za wenyeji,” alieleza na kuongeza kuwa Wachina hawafai kujiingiza katika kazi zinazoweza kufanywa na Wakenya.

Naibu Rais alipongeza uhusiano mzuri baina ya mataifa hayo mawili akisema matarajio ni kwa uhusiano huo kuleta manufaa kwa pande zote, hususan kwa kuzingatia Mkakati Mkuu wa Ushirikiano baina yao uliotiwa saini mnamo 2016 kukuza maendeleo na ustawi.

“China na Kenya zina maono ya pamoja kufanikisha maendeleo na ustawi,” alisema Dkt Ruto, “ambayo yamejumuishwa kwenye mkataba huu unaoshuhudia ubadilishanaji na ushirikiano wa hali ya juu katika miundomsingi, ukuzaji ujuzi, utafiti, teknolojia za habari na mawasiliano (ICT) miongoni mwa mengine,” Dkt Ruto alieleza.

Naibu Rais aliomba wafanyabiashara wa Kenya kutengeneza aina zaidi za bidhaa ili kuziba mwanya wa kibiashara na China.

You can share this post!

Mwanamke amuua mwizi aliyejaribu kumbaka

HUDUMA NAMBA: Baadhi ya watu kusajiliwa upya

adminleo