Sabina Chege: Sababu yangu ya kububujikwa na machozi hadharani
Na NDUNGU GACHANE
MBUNGE Mwakilishi wa Wanawake, Muranga Sabina Chege amefafanua madai kuwa alilia hadharani kwa sababu ya kuzomewa na raia wakati wa mkutano wa vuguvugu la Embrace katika uwanja wa Kimorori, Kaunti ya Muranga Ijumaa.
Bi Chege Jumamosi alieleza kuwa alilia baada ya kupandwa na hisia kwa kuchangamkia yale ambayo serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imewafanyia wakazi wa Murang’a.
“Namkata mtu yeyote mwenye video inayoonyesha nikimzomea aisambaze. Sikuzomewa, nilichangamkia wema na fadhila ambazo Rais ameonyesha kwa kaunti hii. Kupewa mashine za chanjo za thamani ya Sh36 milioni na hundi ya Sh25 milioni kutoka kwa Hazina ya Kustawisha Bishara za Wanawake na Vijana sio mchezo.
“Nilipandwa na hisia kutokana na wema huu nilipogundua kuwa kuna watu ambao bado wanahoji rekodi ya maendeleo ya serikali katika kaunti hii na eneo la Mlima Kenya kwa jumla,” akasema Bi Chege.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri msaidizi wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Bw Rachel Shebesh, Kamishna katika Tume ya Kitaifa ya Jinsia na wabunge wanawake kutoka kuanti mbalimbali nchini.
Akiongea katika Shule ya Msingi ya Kahati ambako alidhamini matibabu ya bure, Bi Chege aliongeza kuwa kando na usaidizi kutoka kwa serikali ya Rais Kenyatta, viongozi wanawake kutoka mseto wa vyama walimsindikiza kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo huku wakimpongeza kwa kazi nzuri.
“Hii haijawahi kufanyika, viongozi walichaguliwa kwa tiketi ya Jubilee, ODM, Wiper, Kanu na vyamba vinginevyo wakitumia jukwaa moja Murang’a kumsifia Rais Kenyatta kwa kazi nzuri ni kitendo cha aina yake. Hii ndio maana niliwaomba vijana wasiniabishe.
“Ni ni kutokana na kisa kimoja katika eneo bunge la Kandara ambako ibada ya Kanisa ilivuruguwa baada ya Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kiambu kuzomewa,” Bi Chege akaeleza.
Mbunge huyo aliwakashifu wanasiasa ambao wamefasiri visivyo hisia zilizomfanya kulia hadharani na kuanza kumkejeli akiwataka kujishughulisha na wajibu wao wa kuwahudumia raia katika maeneo bunge yao.
Kabla ya Bi Chege kuangua kilio jukwaani, Mbunge wa Kigumo Ruth Mwaniki alikuwa amekariri kuwa anamtambua Rais Kenyatta pekee kama kiongozi wa nchini na eneo hilo huku akiuambia umati kwamba atapeleka salamu zao kwake.
Lakini baadhi ya wakazi waliohudhuria mkutano huo walijibu kwa kumwambia mbunge huyo aliwasilisha salamu zao pia kwa Naibu Rais William Ruto.
Mwendo wa asubuhi vijikaratasi vilivyoandikwa “Embrace ni RAO” vilikuwa vimesambazwa katika uwanja huo kuashiria kuwa vuguvugu hilo linadhaminiwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.