Habari Mseto

Sakaja aambia kongamano la Mexico, ‘nilivutiwa mno na maandamano ya Gen Z nchini mwangu’

Na KEVIN CHERUIYOT October 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Kaunti ya Nairobi, Johnson Sakaja, amehimiza taasisi kufanyiwa marekebisho kidemokrasia na usimamizi ili ziwiane na azma ya karne ya 21 kuhusu kuimarisha vijana ambao idadi yao inazidi kukua.

Amesema haya kufuatia maandamano yaliyoshuhudiwa miezi miwili iliyopita, ya kupinga serikali, yaliyovutia jamii ya kimataifa.

Kulingana na Gavana Sakaja, maandamano kama hayo yanachochewa na usimamizi unoawafungia nje vijana wakati wa kufanya maamuzi.

“Viongozi wengi wanahofia vuguvugu la Gen Z. Nilivutiwa mno kwa sababu kwa mara ya kwanza tunawaona vijana ambao wameamua kuacha kulaza damu na kutazama maisha yao yakiwapita,” alisema Gavana Sakaja.

Alisema nguzo kadhaa za kidemokrasia zilibuniwa katika karne ya 19 na zingali zinaendeshwa kupitia mifumo iliyopitwa na wakati.

Alisema haya akihutubu katika awamu ya 11 ya kongamano la Bloomberg CityLab 2024 nchini Mexico, lililowaleta pamoja mameya, waundasera na wataalamu 500 kushiriki mbinu za kutatua matatizo yanayokabili maeneo ya mijini.

“Wakati umefika kutafakari upya taasisi zetu ili zioane na nyenzo na mitazamo ya ulimwengu wa leo. Kwa kufanya hivyo, tutawasirikisha vijana kikamilifu na kusuluhisha changamoto zinazowakabili ikiwemo kubuni suluhu za kudumu,” alisema Bw Sakaja.

Mkuu huyo wa kaunti alisema maandamano yanayoongozwa na vijana ni ishara tosha kuwa vijana wamezinduka na wako tayari kushiriki mchakato wa kufanya maamuzi kama vile kupiga kura na kufanya sauti zao zisikike.

“Wanachosema ni kuwa wanataka kuwa sehemu ya suluhisho. Hautatoa tu misimamo iliyobuniwa na kuwakabidhi. Wanataka kuumba pamoja nawe. Wanataka uwazi kwa njia mpya na ninavutiwa mno kwa sababu hatima ya Afrika ba dunia ipo salama.”

Alisema vuguvugu linaloshuhudiwa ni mwamko mpya kwa viongozi kote ulimwenguni kuwekeza katika vijana kwa kufanyia mabadiliko miradi yao na namna ya kufanya kazi na vijana.

“Wamesema kama hawapo kwenye meza ya mazungumzo, wapo katika kinachozungumziwa, na ikiwa hawapo kwenye meza ya mdahalo hakuna meza, nafikiri huo ni ujasiri mkuu kwa bara la Afrika.”

“Wakati mwingine kama viongozi, tunadunisha mabadiliko yanayotokana na maamuzi madogo tunayofanya, athari inayotokana nayo.”

“Kuondoa marufuku kwamba huwezi ukapiga katikati mwa jiji kuu, majengo ya kihistoria bila kibali, ni moja kati ya maamuzi niliyofanya nilipochukua afisi.”