Habari Mseto

SAKATA YA NYS: Mianya ndani ya mfumo wa IFMIS yalaumiwa kwa wizi

May 29th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

UDHAIFU wa Mfumo wa Usimamizi wa Fedha za Serikali (IFMIS) ndio chanzo kikuu cha kuongezeka kwa wizi wa pesa katika idara mbalimbali za serikali.

Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali, Edward Ouko amesema kwamba idara husika za serikali hazikuzingatia mapendekezo ya afisi yake kurekebisha dosari kadhaa zilizopatikana katika mfumo huo mnamo 2014.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Jumapili jioni, Bw Ouko alisema kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba sakata za ufisadi zinazoiandama serikali kwa sasa zingeepukika ikiwa ushauri wake ungezingatiwa.

“Ni masikitiko kwamba nchi inashuhudia hali ambapo fedha za umma zinapotea kwa njia ambayo ingeweza kuzuiwa. Tuliandaa ripoti ambapo tulitoa ushauri kuhusu matatizo kadhaa yaliyo katika mfumo huo,” akasema Bw Ouko.

Miongoni mwa mapendekezo makuu ya ripoti hiyo ni uwepo wa taratibu kali za usalama ambazo zitawazuia wale ambao hawaruhusiwi na taratibu hizo kuufikia, uwekaji wazi wa taarifa za fedha, uwepo wa taratibu ambazo zitabaini aliyeingia katika mfumo huo kati ya mengine.

Udhaifu huo pia umehusishwa pakubwa na sakata mbili za ufisadi katika Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS) mnamo 2015 na mwaka huu. Katika sakata ya kwanza, zaidi ya Sh1.8 bilioni zinadaiwa kupotea, huku sakata ya sasa ikihisusha kupotea kwa zaidi ya Sh9 bilioni.

Kwa hayo, Bw Ouko alisema kwamba kama njia ya kukabili kupotea fedha, lazima udhaifu huo uzibwe mara moja.

Kwa upande wake, mwanauchumi David Ndii alidai kwamba kuna njama za kimakusudi za baadhi maafisa wakuu serikalini kuuingilia mfumo huo ili kujinufaisha.

Kulingana na Dkt Ndii, haiwezekani kwamba mfumo huo ulipata matatizo hayo bila ufahamu wa maafisa wanaousimamia.

“Ni vipi wizi wa pesa unaweza kutoke bila ufahamu wa maafisa wakuu wa serikali, ambao wanausimamia? Kuna njama fiche katika sakata hizo zote,” akasema.

Hapo Jumatatu, gazeti la Daily Nation lilifichua sakata nyingine ambapo Sh2 bilioni zinashukiwa kuibwa kwenye mradi wa kupanda miti katika taasisi za elimu kote nchini.

Hii inaongezea kwenye sakata ndani ya serikali, nyingine ikiwa ni ya mahindi katika bodi ya NCPB.