• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
SARATANI YA MATITI: ‘Nilidhani ni ugonjwa wa wanawake pekee…’

SARATANI YA MATITI: ‘Nilidhani ni ugonjwa wa wanawake pekee…’

NA PAULINE ONGAJI

Alipogundua kwamba alikuwa anaugua kansa ya matiti mwaka jana, alishtuka sana kwani hakujua kwamba maradhi haya pia huwakumba wanaume.

Lakini ni uhalisia ambao Charles Maina, 60, mkazi wa eneo la Kieni, Kaunti ya Nyeri, alilazimika kukumbatia, suala ambalo limemwezesha kufuatilia matibabu vilivyo.

Masaibu ya Bw Maina yalianza Agosti 31, mwaka jana. “Nilianza kukumbwa na maumivu makali kwenye titi langu la kushoto. Mwanzoni nilidhani yalikuwa tu maumivu ya kawaida, lakini uchungu ulipozidi, nikaamua kwenda hospitalini,” aeleza.

Kulingana naye, madaktari walikabiliwa na changamoto ya kubaini nini hasa kilichokuwa kikimtatiza. “Si mara moja waliniambia kuwa huenda maumivu yanatokana na mafuta mwilini, hasa ikizingatiwa kwamba wakati huo nilikuwa mnene,” asema.

Anasema kwamba alipewa dawa ya kukabiliana na maumivu na kuruhusiwa kurudi nyumbani. Hata hivyo, kufikia Desemba mwaka jana, hali ikawa tete kwani ule uchungu ulikuja kwa mshindo, hivyo ikabidi arudi hospitalini kwa uchunguzi zaidi.

“Wakati huu madaktari walichukua muda wao kufanya chunguzi kadha wa kadha ila bado tatizo halikubainika mara moja. Uchunguzi huu uliendelea kwa muda huku madaktari wakitumia mbinu ya ultrasound-guided needle biopsy, na kufikia mwisho wa Februari mwaka huu, waliweza kutambua kwa kweli ilikuwa kansa ya matiti,” anasema.

Lakini kwa bahati mbaya maradhi haya yalikuwa tayari yameenea hadi kwenye mapafu na wakamshauri kuanzisha matibabu mara moja.

“Mwezi Machi mwaka huu, nilianza rasmi matibabu ya dawa hadi Juni. Nilikuwa nimeanza kupata nafuu angaa kulingana na uchunguzi uliofuatia lakini kufikia Septemba, kidonda kikachipuka kifuani. Nilipoenda hospitalini, nilianzishiwa matibabu ya tibaredio mara moja, ambapo nilikamilisha kikao cha mwisho wiki tatu zilizopita,” aeleza.

Kwa sasa amemaliza vikao kumi vya tibaredio na anajiandaa kuanza matibabu ya tibakemia.Japo Bw Maina ana matumaini kwamba yuko katika mkondo mwema kimatibabu kwani hali yake imekuwa ikiimarika, haijakuwa rahisi kwani mbali na mzigo wa kifedha unaotokana na gharama za matibabu, haikuwa rahisi kukubali kwa kweli alikuwa anaugua kansa ya matiti.

“Unapofichua habari kwamba unaugua kansa ya matiti; ugonjwa unaofahamika kuwakumba hasa wanawake, sio rahisi watu wakuelewe. Wengi waliotambua kuhusu hali yangu, mwanzoni hawakuamini,” aeleza.

Na ndiposa amejitokeza na kutangaza hali yake ili kuwapa wanaume wengine wanaogua maradhi haya nguvu ya kujitokeza waweze kupokea matibabu mapema.

“Hakuna nafasi ya aibu tena. Ukisikia kuna shughuli ya kupima watu, kama mwanamume jitokeze. Kuwa na mazoea ya kukagua sehemu hii hata kama waona sio jambo la kawaida,” aeleza.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani- WHO, japo kansa ya matiti ni nadra mno miongoni mwa wanaume ikilinganishwa na wanawake, sio jambo la kupuuzwa.

Kwa makadirio ya WHO, takriban visa 2,620 vya kansa ya matiti kwa wanaume vilitarajiwa mwaka huu nchini Amerika, huku takriban vifo 520 vikitarajiwa kutokana na ugonjwa huu.

Hapa nchini hakuna takwimu kamili zinazoonyesha idadi ya wanaume wanaougua maradhi haya.Dkt Miriam Mutebi, daktari wa upasuaji wa kansa ya matiti katika hospitali ya Aga Khan, anasema kwamba sawa na wanawake, ishara za kansa ya matiti kwa wanaume ni pamoja na uvimbe usio na uchungu kwenye tishu ya matiti huku ngozi inayozingira titi lililoathirika ikibadilika rangi na kuwa nyekundu na kuonekana kana kwamba ina magamba.

“Pia, chuchu hubadilika na kuwa nyekundu na kuonekana kana kwamba ina magamba au kuanza kubadili na kuingia ndani ya ngozi,” aeleza.

Kulingana na WHO, ili kuongeza uwezekano wa mgonjwa kupona na hivyo kuzuia vifo, utambuzi wa mapema ni muhimu.Kuna mikakati miwili ya utambuzi wa kansa ya matiti.

Moja yazo ni utambuzi wa mapema na hivyo kuanzisha tiba haraka iwezekanavyo. Kisha kuna uchunguzi ili kutambua kansa kabla ya ishara kujitokeza (screening), ambapo ala za utaratibu huu zinahusisha mammography, kukaguliwa titi na mhudumu wa afya, na wewe mwenyewe kujikagua titi lako.

Lakini japo mbinu hizi zimesaidia wanawake wengi kutambua mapema maradhi haya na hivyo kuyadhibiti, huenda ukawa mlima mrefu kukwea kwa wanaume.

“Sio rahisi kwa wanaume kukubali au hata kufikiria kufanyiwa taratibu hizi, na hili ni tatizo katika vita dhidi ya maradhi haya miongoni mwa wanaume,” aeleza Catherine Wachira, Mwenyekiti wa shirika la Kenya Network of Cancer Organization.

Kulingana na Bi Wachira, changamoto kuu imekuwa kuwarai wanaume kufanyiwa uchunguzi wa matiti, ili kutambua maradhi haya mapema na kuanza matibabu kabla kuenea katika sehemu zingine mwilini.

“Tatizo ni kwamba wanaume wengi wanaogopa kujitokeza kwani wanachukulia kuwa ugonjwa wa wanawake,” aeleza Bi Wachira.Kulingana na Dkt Mutebi, kuna haja pia ya kuhamasisha wanaume kuhusu mambo yanayoongeza hatari ya kukumbwa na maradhi haya, na hivyo kuyaepuka baadaye.

Nini kinachoongeza hatari ya kukumbwa na saratani ya matiti kwa wanaume?

Dkt Mutebi kuna mambo kadha wa kadha ambayo huongeza hatari ya kukumbwa na maradhi haya miongoni mwa wanaume, ikiwa ni pamoja na umri, ambapo waathiriwa wa kansa ya matiti miongoni mwa wanaume huwa katika miaka ya sitini.

Pia anataja historia ya maradhi haya katika familia ambapo ikiwa una jamaa wa karibu ambaye amewahi ugua kansa ya matiti, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuugua pia.

“Katika mataifa ya magharibi, imekadiriwa kwamba 10% ya wanaume wanaougua kansa ya matiti wana historia ya kifamilia ya kansa ya matiti au ya ovari. Pia, hali kama vile BRCA2 mutation and Klinefelter’s Syndrome (XXY) zinaongeza hatari, japo kinachochangia masuala haya ya kijenetiki barani Afrika, bado hakijatambulika,” anaeleza Dkt Mutebi.

Anasema kwamba kuna sababu zingine zinazosababisha mabadiliko ya matiti kwa wanaume kama vile ugonjwa wa gynaecomastia (ambapo matiti yanakuwa makubwa kutokana na sababu kadha wa kadha), kumaanisha kwamba ili kuwa kuwa salama, mabadiliko haya yanapaswa kukaguliwa na daktari.

Kulingana naye, kuna masuala yanayoweza kubadilishwa na kuna yale hayawezi kubadilishwa. “Kwa mfano haiwezekani kwa mtu kubadili historia ya familia yake, au aepuke uzee – baadhi ya masuala yanayochangia pakubwa hatari ya aina hii ya kansa. Lakini kuna mambo ambayo waweza badilisha kupunguza hatari hii. Mbinu mwafaka asema ni kubadili mtindo wa maisha kwa kula chakula chenye afya na kufanya mazoezi,” asema.

Kwa wanaume, aidha aongeza kuwa, kuna uwezekano wa kansa ya matiti kuenea kwa kasi katika sehemu zingine mwilini kwani tishu za matiti yao ni ndogo ikilinganishwa na wanawake, na ndiposa kansa ya matiti miongoni mwa wanaume huja kwa mshindo na ni rahisi kusambaa mapema.

“Tiba huhusisha upasuaji wa kuondoa tishu za titi lilioathirika, lakini pia kuna matibabu mengine kama vile tibakemia na tibaredio kuambatana na hali ya mwathiriwa. Sawa na aina nyingine za kansa, utambuzi wa mapema, ndio siri kuu ya kuimarisha uwezekano wa kupona baada ya kupokea matibabu,” asema Dkt Mutebi.

Mtaalamu huyu anasema kwamba waathiriwa wa kiume wa kansa ya matiti huenda wakahitajika kupokea matibabu yanayolengewa homoni za kike mwilini mwao, suala ambalo huwatia wengi aibu.

“Hii inamaanisha kwamba wanahitaji usaidizi hata zaidi katika safari hii ya matibabu,” aongeza.Kulingana na Bi Wachira, haya ni masuala ambayo wanaume wengi hawafahamu, kumaanisha kwamba hawana habari hata wanapokumbwa na hatari ya kiafya.

“Ndiposa shughuli za uhamasishaji miongoni mwa wanaume zinapaswa kushika kasi. Wanaume wanahitaji utambuzi wa mapema na kuhamasishwa kuhusu jinsi ya kukagua sehemu hii ya mwili, ili iwe kawaida kwao kufanya hivyo bila aibu,” asisitiza.

You can share this post!

Corona ilitufungua macho, sasa tunavuna maelfu kwa biashara...

WANDERI KAMAU: Ufalme huenda ukarejesha siasa komavu...