Sehemu iliyokuwa imegeuzwa dampo hatari Githurai 44 yaokolewa
Na SAMMY WAWERU
HATIMAYE eneo lililokuwa limegeuzwa dampo mtaani Githurai 44 katika Kaunti ya Nairobi kwa muda mrefu limetwaliwa serikali ikiokoa sehemu hiyo dhidi ya uchafuzi.
Jaa hilo lililoko kati ya mto unaogawanya Kaunti ya Nairobi na Kiambu na ilipokuwa afisi ya mmoja wa machifu wa Githurai, lilikuwa hatari kwa maisha ya wakazi.
Mbali na kutumika kama mtandao wa kuchafua mazingira, lilikuwa na mitaro na mashimo yaliyoteka maji msimu wa mvua, jambo lililozua hatari hasa kwa watoto.
Usiku, lilikuwa hatari kwa wapita-njia kwa kinachosemekana kuwa maficho ya wahalifu na wahuni.
Isitoshe, lilichangia kuzaana na kusambaa kwa wadudu hatari aina ya mbu, kutokana na taka zilizotupwa humo.
Hatua ya kutwaa dampo hilo, imejiri miezi kadhaa baada ya Taifa Leo kuliangazia.
Wiki chache zilizopita, kiasi kikubwa cha taka zilizotupwa humo zilizolewa na kuzingirwa kwa ua ya nyaya na fito, duru zikiarifu hatua hiyo ilitekelezwa na uongozi wa wadi ya Githurai.
“Hatujaarifiwa ni mradi upi wa maendeleo unaopaniwa kufanyika hapa. Tunaomba uwe utakaotufaidi,” Francis Munene, mmoja wa mkazi eneo akasema kwenye mahojiano.
Kulingana na mkazi huyo, ingekuwa busara iwapo serikali ya Kaunti ya Nairobi ingejenga maduka na kuyakodi, akieleza itanufaisha watakaowekeza katika biashara na pia serikali kupitia ukusanyaji wa kodi na ulipaji wa leseni ya kuhudumu.
Eneo la Githurai halina uwanja maalum wa watoto, wanafunzi na vijana kuchezea.
“Vipaji wetu wa soka Githurai hawana uga kufanyia mazoezi. Tumehangaika kwa muda mrefu, na tunasihi serikali ya kaunti kugeuza eneo hilo kuwa uwanja,” Patrick Ogwayo, mmoja wa mkufunzi wa Githurai United na All Stars Githurai amependekeza.
Ukosefu wa eneo maalum watoto na vijana kuchezea Kaunti ya Nairobi unaendelea kuwa kikwazo katika mitaa mbalimbali.
Eneo lililotwaliwa Githurai ni ardhi ya umma.
Shughuli hiyo imetekelezwa wakati ambapo serikali inaendelea ardhi zilizonyakuliwa Nairobi na sehemu mbalimbali nchini.