SENSA: Kina mama 180,000 hujifungulia nyumbani
Na PETER MBURU
LICHA ya mpango wa serikali wa afya kwa wote na kuondoa mfumo wa kulipisha kina mama wanaotafuta huduma za kujifungua hospitalini, bado kuna wanawake wengi wanaojifungulia nyumbani.
Kulingana na ripoti iliyotolewa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), kati ya wanawake 1,340,468 waliojifungua kwa kipindi cha mwaka hadi sensa ilipofanywa Agosti 2019, 189, 464 hawakupata huduma hizo katika vituo vya afya.
Vilevile, kati ya idadi hiyo, kina mama wapatao 2,297 waliripoti kuwa hawakuwa wakijua walipojifungulia.
Takwimu za KNBS aidha zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita watoto wapatao 763,452 wamezaliwa mahali ambapo si katika vituo vya afya, huku watu 9,590 wakikosa kufahamu walijifungulia wanao wapi.
Maeneo yaliyoadhirika na hali hii zaidi ni mashambani, ambapo watoto 173,847 hawakuzaliwa hospitalini kwa kipindi cha mwaka hadi Agosti, 2019 na watu 2,031 hawakufahamu walipojifungulia.
Kaunti ya Mandera inaongoza kwa idadi ya watu ambao hawajifungulii katika vituo vya afya kwani kwa miaka mitano iliyopita, watoto wapatao 41,071 wamezaliwa nje ya vituo vya afya. Kwa mwaka mmoja, watoto 12, 463 walizaliwa nje ya vituo vya afya, kati ya idadi jumla ya watoto 26,639 waliozaliwa.
Kulingana na idadi ya watoto waliozaliwa kwa mwaka mmoja, Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa kurekodi watoto 135,229, ikifuatwa na Kiambu kwa watoto 69,596.
Katika kaunti hizo mbili, watoto 2,206 na 1,705 mtawalia walizaliwa nje ya mahospitali.
Kaunti za Lamu na Isiolo nazo zilirekodi idadi ndogo zaidi ya watoto waliozaliwa, kwa visa 4,235 na 8,037 vya kujifungua mtawalia. Watoto 756 Lamu walizaliwa nje ya vituo vya afya, nako Isiolo watoto 2,333 wakazaliwa bila huduma za hospitali.