Serikali yatakiwa kuwapa raia pesa badala ya chakula
Na WANDERI KAMAU
MAGAVANA nchini wanaitaka Serikali kuwapa Wakenya pesa kujinunulia chakula wenyewe, ili kuepuka hali ambapo misongamano inaweza kutokea watakapoenda kuchukua misaada itakayotolewa na serikali.
Kupitia kwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya, wakuu hao wa kaunti walisema kuwa hali hiyo itawapa wananchi uhuru wa kujinunulia chakula wanachotaka, badala ya kulazimika kutumia kile wanachopewa na serikali.
Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, Bw Oparanya alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha kuwa maagizo ya serikali kuhusu kutokaribiana ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona yamezingatiwa.
Kauli yake imejiri baada ya serikali kusema Jumatatu kwamba imetenga Sh40 bilioni kuwasaidia watu maskini, hasa katika maeneo ya mijini kupata chakula kutokana na athari za virusi hivyo.
“Tunaunga mkono hatua ya serikali kutangaza kuwa itazisaidia familia hizo. Hata hivyo, tunaomba mpangilio mpya kuhusu jinsi utaratibu wa usambazaji chakula utafanywa. Hili ni kwa kuhakikisha kwamba hakuna mkanyagano unaotokea wakati wa kusambaza chakula hicho,” akasema Bw Oparanya.
Mwenyekiti huyo alirejelea kisa cha wiki iliyopita mjini Eldoret, ambapo mbunge wa Kesses Swarup Mishra, alizuiwa kutoa chakula cha msaada kwa wakazi wa eneobunge hilo kutokana na hofu ya kuzuka kwa mkanyagano.
“Itakuwa hatua nzuri sana kwa serikali kuwapa chakula wananchi. Hilo pia litawapa wananchi uhuru wa kujinunulia chakula wanachokitaka, kwani inaweza kuwapa mahindi wakati wanataka viazi,” akasema Bw Oparanya, ambaye pia ndiye gavana wa Kakamega.
Wakati huo huo, baraza hilo lilifutilia mbali kongamalo la ugatuzi ambalo lilikuwa limepangwa kufanyika katika Kaunti ya Makueni kati ya tarehe 20 na 23 mwezi huu.
Kongamano hilo ndilo lingekuwa la saba tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi nchini mnamo 2013.
Zaidi ya hayo, kauti zilitangaza kuanza harakati za kuwaajiri wahudumu wa afya 5,500 kama zilivyoagizwa na serikali kuu, ambapo wanatarajiwa kuanza kazi Alhamisi wiki ijayo ili kupiga jeki harakati za kukabiliana na virusi vya corona.
Vile vile, alieleza kuwa kaunti zote zishatimiza agizo la Wizara ya Afya la kutenga angaa shule 20 za mabweni, ambazo zitatumika kama maeneo ya kuwahifadhi watu wanaotengwa kwa kuhofiwa kuambukizwa virusi hivyo.
Mwenyekiti huyo pia aliondoa hofu kwa Wakenya wanaougua maradhi mengine, akisema kwamba wataendelea kupokea matibabu kama kawaida katika hospitali za kaunti.
Hii ni kufuatia hofu kuwa juhudi zote zinaelekezwa katika kukabiliana na corona huku walio na maradhi mengine wakipuuzwa.