Habari Mseto

Serikali yatoa magunia 600,000 kupunguza bei ya unga

June 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Hifadhi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB) imetoa magunia 600,000 ya mahindi kwa wasagaji wa unga baada ya serikali kuu kuingilia kati.

NCPB ilikuwa imechelewa kutoa mahindi hayo licha ya wafanyibiashara kulipia nafaka hiyo Sh1 bilioni mwezi mmoja uliopita.

Kufikia Ijumaa wiki iliyopita, NCPB ilieleza kuwa watengenezaji unga walikuwa wameanza kuchukua bidhaa hiyo. Magunia zaidi yatachukuliwa juma hili, ilisema NCPB.

Kulingana na meneja wa mawasiliano wa NCPB Titus Maiyo, mahindi yalianza kuchukuliwa Jumatatu, wiki moja baada ya mkuu wa huduma za umma Joseph Kinyua na Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kuendesha mkutano kusuluhisha mgogoro kati ya NCPB na kamati ya hifadhi ya chakula cha dharura (SFR).

Serikali ilisimamisha kutolewa kwa mahindi hayo baada ya madai kuibuka kuwa baadhi ya watengenezaji walikuwa wakitaka kununua bidhaa hiyo kwa bei ya chini kwa lengo la kujinufaisha kibiashara.

“Watengenezaji wa mahindi wameanza kuchukua mahindi na kufikia sasa wamechukua magunia 400,000 na magunia zaidi yanatarajiwa kuchukuliwa wiki hii,” alisema Bw Maiyo.

Serikali inatarajiwa kutoa magunia milioni tatu ya mahindi kwa wasagaji kwa lengo la kukabiliana na gharama ya juu ya unga wa mahindi ambao kwa sasa unauzwa kwa Sh120 kwa pakiti ya kilo mbili.

Serikali inauza gunia la kilo 90 kwa Sh2,300 dhidi ya thamani yake katika soko huru ya Sh3,300.