Serikali yatoa tahadhari mpya kuhusu Ebola
Na WAIKWA MAINA
SERIKALI imetoa tahadhari mpya kuhusu mkurupuko wa Ebola baada ya ugonjwa huo kuripotiwa katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).
Ilani hiyo ilitolewa na Wizara ya Afya Agosti 6, kwa kaunti zote na wasimamizi wa afya bandarini. Pia litoa nambari maalumu ambayo maafisa wanafaa kupiga ripoti endapo watagundua kuna mtu mwenye ugonjwa huo hatari.
Mkurupuko wa Ebola ulitangazwa katika Mkoa wa Kivu Kaskazini, uliopo mashariki mwa DRC.
Maafisa wa afya walishauriwa kuwa waangalifu ili watambue maradhi au vifo visivyoeleweka katika jamii.
Kulingana na Kaimu Mkurugenzi wa Afya, Dkt Patrick Amoth, mkurupuko huo ulitangazwa Agosti 1, wiki moja baada ya wizara ya afya ya DRC kutangaza kuwa mkurupuko ulikuwa umedhibitiwa katika Mkoa wa Equateur ulio magharibi mwa DRC, kilomita 2,500 kutoka Kivu Kaskazini.
Wizara hiyo ilifahamisha Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kwamba kati ya majaribio sita yaliyofanywa katika Taasisi ya Utafiti wa Matibabu iliyo Kinshasa, manne yalithibitisha ni virusi vya Ebola lakini utafiti zaidi unaendelezwa.
Dkt Amoth alisema Kivu Kaskazini ni eneo linalopakana na Rwanda na Uganda ambapo kuna vita, na watu zaidi ya milioni moja walioachwa bila makao.
Aliongeza kuwa eneo hilo hupitiwa na wafanyabiashara, waendeshaji malori ya mizigo na wakimbizi.
“Zaidi ya hayo, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) ni sehemu muhimu inayounganisha ukanda wa Afirika Mashariki na ya Kati,” akasema.
Aliagiza maafisa wote wa afya nchini wazidishe ukaguzi wa kiafya ili kuzuia ueneaji wa Ebola nchini.
“Mikakati itakayochukuliwa inafaa kuwezesha utambuzi wa mapema, utoaji ilani na uchukuaji wa hatua mwafaka za kudhibiti tukio lolote katika sehemu zote za afya Kenya, kuanzia mashinani hadi katika hospitali za kitaifa za rufaa na mipaka yetu,” akasema.
Wasimamizi wa afya katika kila kaunti, kaunti ndogo, hospitali na wale walio katika maeneo ya mipaka watatakikana kukusanya habari za kina kuhusu wasafiri wote wanaotoka DRC katika kila kiingilio mipakani.
Watahitajika pia kuwa macho ili wabainishe kama kuna yeyote aliye na joto kali mwilini kupita kiasi na kama mtu amewahi kupitia DRC au kuwa karibu na mtu aliyekuwa DRC katika wiki tatu zilizopita.
Wasimamizi wa afya katika kaunti ndogo walishauriwa kuimarisha ukaguzi wa kiafya vijijini na kuhakikisha wafanyakazi wote wa matibabu wanafahamu kuhusu hatari ya mkurupuko wa Ebola nchini.
Walitakiwa pia kuhusisha wadau wote husika katika shughuli hii zikiwemo taasisi za usalama, hospitali za kibinafsi, mashirika ya kijamii na mashirika mengine yanayohusika katika uhamasishaji wa masuala ya kijamii.