• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
SHAIRI: Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri

SHAIRI: Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri

Na KULEI SEREM

Wahadhiri nina  swali, mtagoma hadi  lini?,
Ni kama hamtujali, sasa twaenda nyumbani,
Kweli mbaya zetu hali, tumekosa tumaini,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.

Migomo ya kila mwaka, inatukula mahini,
Wanafunzi tumechoka, na mambo yalo vyuoni,
Twatamani kuondoka, elimu kuweka chini,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.,

Twapenda sana elimu, kwa dhati tunaienzi,
Tunajua ni muhimu, tukakuwa wanafunzi,
Hatuwezi kujikimu, kwa maisha ya kiinzi,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.

Elimu ni ghali mno, sisi twasoma kwa shida,
Nyumbani hamna vuno, labda ugali wa bada,
Taabu mambo ya wino, heri kuwa bodaboda,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.

Tunataka kuhitimu, muda wetu wayoyoma,
Inatukimbia damu, tunang’ang’ana kusoma,
Kufaidi kwa elimu, wahadhiri wanagoma,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.

Wakisema viongozi, mwanzo wa ngoma ni lele,
Kazini hakuna pozi, elimu kipaumbele,
Wahadhiri kwa machozi, barabarani kelele,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.

Mwakanyaga kama lapa, wahadhiri mnanyenga,
Madeni yale kulipa, ni kuzito kama nanga,
Harusi kweli kukopa, kulipa ndiko matanga,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.

Mwasema hakuna pesa, ila mnaficha siri,
Mwatuza wanasiasa, wabunge na mawaziri,
Kwa hakika inatesa, ni chungu kama shubiri,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.

Wahadhiri wanalia, wana lindi la mawazo,
Kazini wanaumia, njiani vingi vikwazo,
Mara kiguu na njia, yasemwa mazungumzo,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.

Iwapo hamtalipa, sisi tutahadhirika,
Wenzetu wanywa kwa chupa, maisha yaharibika,
Riziki zetu mapipa, kwa kuzoea takataka,
Serikali tunaomba, muwalipe wahadhiri.

MALENGA KULEI SEREM

You can share this post!

KRU yatangaza kikosi cha wachezaji 35 wa Simbas 2018

SHAIRI: Ushairi tujifunze, tupate kuumaizi

adminleo