SHANGAZI: Nimegawia wengi asali lakini sijawahi kuhisi utamu
Na SHANGAZI SIZARINA
Shikamoo shangazi. Nina umri wa miaka 28 na nimekutana na wanaume kadhaa tangu nijue masuala ya mahaba. Ajabu ni kuwa sijawahi kufurahia utamu wa burudani hata siku moja. Je, nina kasoro?
Kupitia SMS
Kusema kweli sijawahi kukutana na mtu mwingine aliye katika hali kama hiyo yako. Wengi wao hasa hulalamika kwamba hawatosheki. Inawezekana kwamba unaokutana nao hawana ujuzi unaohitajika kusisimua hisia zinazoleta utamu wa shughuli hiyo. Kuwa na subira, siku moja utakutana na pwaguzi akushughulikie ipasavyo.
Hana muda wa kusema nami
Hujambo shangazi. Nilikuwa na mpenzi na nikaenda kazi mbali. Nikiwa huko alikuwa akinipigia simu kuniambia jinsi anavyonipenda na hata kuniahidi kuwa tutaoana. Nilirudi majuzi kwa likizo na nilipompigia simu akakata na kunitumia SMS akisema hana wakati wa kuongea nami. Baadaye nilimpigia simu akazima. Nifanyeje?
Tabia ya mpenzi wako ni ishara kwamba hataki tena uhusiano kati yenu. Kuna uwezekano mkubwa kwamba alishikana na mwanamume mwingine ulipokuwa mbali naye. Mapenzi hayalazimishwi kwa hivyo itabidi ukubali uamuzi wake.
Amenizidi umri, je nimkubali?
Shangazi nina mpenzi lakini kuna jambo linalonitia wasiwasi. Amenizidi umri kwa mwaka mmoja na ninashangaa iwapo ninaweza kuoa mwanamke mwenye umri mkubwa kunishinda. Nishauri.
Nimesema mara nyingi katika safu hii kuwa umri si hoja sana wawili wanapopendana. Isitoshe, tofauti ya mwaka mmoja ni ndogo sana na hilo si jambo linalofaa kukutia wasiwasi. Ondoa hofu na ushughulikie uhusiano na ndoa yenu.
Rafiki alimnyaka sasa wameachana
Vipi shangazi. Kuna msichana niliyempenda lakini akanyakuliwa na rafiki yangu kabla sijamdoekezea hisia zangu kwake. Sasa wameachana na bado nampenda. Ninajua pia nikimwambia nampenda atanikubali. Nishauri.
Kupitia SMS
Sijui unahitaji ushauri gani ilhali kila jambo liko wazi kutokana na maelezo yako. Unasema kuwa wameachana sasa hana mpenzi, bado unampenda na una hakika ukimwambia atakubali. Unangoja nini? Ukizubaazubaa atanyakuliwa tena. Shauri yako.
Hakutaka nijulikane na watu wa kwao
Shangazi pokea salamu zangu. Ni mwaka mmoja sasa tangu nilipooa. Ajabu ni kuwa mke wangu huwa hataki jamaa zake wajue kuwa ameolewa. Amekuwa akiwadangaya yuko kazini na pesa anazowatumia huwa zinatoka kwangu. Juzi alisafiri kwao na amekataa kurudi. Nifanye nini?
Ukweli ni kuwa huyo unayemuita mke wako hakupendi bali alikuchezea akili tu ili kwanza avune pesa kutoka kwako. Ndiyo maana hakutaka ujulikane kwao wala jamaa zake wajue kuwa ameolewa kwa sababu hiyo haijawa nia yake kwako. Kama ameenda kwao na amekatalia huko, usimngojee kwani hatarudi. Ameshapata alichokuwa akitaka kutoka kwako.
Mamake anapinga
Shikamoo shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 20 na mpenzi wangu ana miaka 21. Yeye yuko tayari kunioa lakini mama yake anapinga akisema bado hajafikisha umri. Nifanye nini?
Mimi pia nahisi ni mapema kwa mwanamume huyo kuoa kwani bado hajakomaa kiakili kiasi cha kuweza kushughulikia masuala ya ndoa. Labda pia hana uwezo wa kukimu familia na ndiyo maana mama yake anapinga. Ikiwezekana subiri labda afikishe angalao miaka 25.
Nampa pesa lakini hanipakulii
Shikamoo shangazi? Mimi nina mpenzi lakini nimegundua kuwa haja yake kwangu ni pesa tu hakuna mapenzi. Nikimuomba asali anaruka. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS
Kama huna habari, si lazima mwanamke akulambishe asali ili kuthibitisha penzi lake kwako. Tendo hilo hasa linafaa kusubiri hadi watu wanapooana. Hata kama unampa pesa mpenzi wako, unafanya hivyo kwa hiari wala si kumhonga ili akulambishe asali. Ukihisi kwamba anakutumia vibaya acha kumpa pesa ama uachane naye.