Habari MsetoSiasa

Sheria ya refarenda yaandaliwa

November 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA DAVID MWERE

DALILI ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi zinazidi kudhihirika baada ya wabunge kuanza mchakato wa kuunda mswada ambao ukipitishwa, utatoa nafasi ya kura hiyo ya maoni kufanyika.

Hatua hiyo inajiri huku Jopokazi la Maridhiano maarufu kama BBI likitarajiwa kuwakabidhi Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa upinzani Raila Odinga ripoti yao wiki hii.

Ripoti ya BBI inatarajiwa kupendekeza vifungu vya katiba ambavyo vinafaa kubadilishwa kupitia kura hiyo ya maamuzi.

Kenya imekuwa na refarenda mbili, moja iliyoandaliwa mwaka wa 2005 lakini ikakosa kupitishwa baada ya kukataliwa na Wakenya.

Hata hivyo, jaribio la pili la mwaka wa 2010 lilizaa matunda ikizingatiwa Rais Mstaafu Mwai Kibaki wakati huo akiwa afisini na Bw Odinga akiwa Waziri Mkuu waliungana na kuvumisha wito wa kupatikana kwa katiba mpya hasa baada ya uchaguzi tata wa 2007.

Mswada wa sasa unaodhaminiwa na mbunge wa Ndaragwa Jeremiah Kioni ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Inayosimamia Utekelezaji wa Katiba (CIOC) unatoa jukwaa bora la kuandaliwa kwa kura ya maamuzi.

“Mswada huu unatoa mwongozo mahususi wa kuandaliwa kwa kura ya maoni, utaratibu wa kufuata na masuala ya kushughulikiwa,” ukasema mswada huo.

Hata hivyo, maswali yameibuliwa kuhusu mswada wenyewe kwa kuwa hauonyeshi namna ya kuhakikisha kwamba uchaguzi huru unaandaliwa.

Vilevile mswada huo haufafanui iwapo mswada wa mwisho wa kupigiwa kura ya refarenda unafaa kufanyiwa marekebisho na bunge ama unafaa kushughulikiwa na kamati ya wataalamu kabla ya kufikishwa kwenye mabunge ya kaunti.

Huenda mswada huo ukakabiliwa na hali sawa kama ule wa Punguza Mizigo ambao ulifeli baada ya kukosa kupata uungwaji mkono kwenye mabunge ya kaunti baada ya kupendekeza kupunguzwa kwa idadi ya viti vya ubunge.

Ingawa hivyo, katiba inasema kwamba marekebisho ya sheria inafaa kutekelezwa baada ya mswada wenyewe kutiwa saini na wapigakura wasiopungua milioni moja huku mchakato wa kuthibitisha saini hizo ukichukua siku 90.