Habari Mseto

Shirika lafichua miradi inayopendekezwa na wakazi hupuuzwa

March 5th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na OSCAR KAKAI

RIPOTI ya shirika lisilo la serikali katika kaunti ya Pokot Magharibi inaonyesha kuwa vyama vya kisiasa katika serikali iliyopita vilikuwa vikibadilisha miradi ambayo ilikuwa imependekezwa na kupewa kipaumbele na wakazi.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa wawakilishi wa wadi katika bunge la kaunti hiyo walikuwa wakibadilisha miradi kulingana mirengo yao ya kisiasa ili kujinufaisha.

Akiongea katika mkutano wa mwaka wa Speaking Pokot Accountability Network, katibu wa shirika hilo Bw Francis Soprin, alisema kuwa serikali  iliyopita ilikuwa ikishirikisha wakazi kupendekeza miradi za kupewa kipaumbele  na baada ya wao kutoa mapendekezo miradi hiyo ilikuwa ikibadilishwa.

“Watu wachache walikuwa wakishirikishwa kuchagua miradi ambayo inawafaa lakini baada ya mchakato huo  wawakilishi wa kaunti walikuwa wakibadilisha ili iwiane  na matakwa yao ya kisiasa.

Bw Soprin alisema kuwa hali hii imewapa changamoto kushinikiza serikali ya kaunti ya sasa kuunda  mswada wa kushirikisha umma ili kuhakikisha mapendekezo ya miradi  yanatekelezwa.

“Mswada huo utasaidia wakazi kuhusishwa kikamilifu kupendekeza miradi ambayo wanaipa kipaumbele ili itekelezwe,” alisema.

 

Mafunzo

Katibu huyo alisema kuwa wametoa mafunzo kwa mtu mmoja katika kila wadi kwenye  wadi zote ishirini za kaunti hiyo ili kuwa wachunguzi wa  kijamii wanaopiga msasa na kuchunguza miradi ambayo inatekelezwa na serikali za kaunti na kitaifa.

“Wakenya wanalipa ushuru ili kufadhili miradi hiyo. Tunataka kuwa na watu mashinani ambao wanafuatilia na kuchunguza ikiwa matakwa yao yanatimizwa,” akasema.

Alidai kuwa shirika lake limepokea vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi, wakati wa kufuatilia miradi baada ya kupata ripoti kutoka kwa wachunguzi wa kijamii.

Bw Soprin alipongeza serikali ya sasa ya kaunti hiyo kwa kutoa  ufadhili wa wanafunzi  kwa usawa.

Bi Salome Chepkemei  afisa wa shirika hilo alizitaka serikali za kaunti na kitaifa kuhakikisha kuwa asilimia 30  ya zabuni zinapeanwa na akina mama na vijana kulingana na katiba.

“Serikali hizi mbaili zinafaa kuhakikisha kuwa kuna uwazi wakati wakutekeleza miradi zao.