Habari Mseto

Shule ya umma yaagizwa ihame ardhi inayozozania na kampuni ya mwanasiasa

Na VITALIS KIMUTAI October 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SHULE ya msingi ya umma katika manispaa ya Bomet imepoteza ardhi ya ekari 10.6 inayomiliki kufuatia uamuzi wa mahakama uliounga mkono kampuni inayohusishwa na aliyekuwa mgombeaji wa ugavana na mfanyabiashara.

Shule ya Msingi ya St Michael’s imeagizwa na Mahakama ya Mazingira na Ardhi huko Kericho kuondoka katika ardhi iliyo karibu na Chuo Kikuu cha Bomet ndani ya siku 45.

Mahakama iliamua kwamba ardhi hiyo ni ya Taasisi ya Kiufundi ya Bomet, inayofanya biashara kama Lomu Investments, kampuni inayomilikiwa na Bernard Mutai Chepkwony.

Bw Chepkwony aligombea kiti cha ugavana Bomet bila kufaulu kwa tikiti ya chama cha Amani National Congress (ANC) katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Jaji M.C. Oundo aliagiza kwamba shule hiyo pia lazima ilipe Lomu Investments Sh2 milioni kama fidia kwa kuingia kimakosa kwenye ardhi hiyo, akisema kuwa kampuni hiyo ndiyo iliyosajiliwa kisheria kama mmiliki wa mali hiyo.

“Hakukuwa na ushahidi uliotolewa kwamba mlalamishi [Lomu Investments] alipata ardhi kwa njia ya ulaghai au kwamba cheti chake cha kukodisha kilipatikana kwa njia haramu, bila utaratibu, au kupitia mpango wa ufisadi,” Jaji Oundo aliamua.

Wazazi katika Shule ya Msingi ya St Michael, hata hivyo, wameapa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama na kupigania kuhifadhi umiliki wa ardhi hiyo.

Mwishoni mwa juma walifanya mkutano maalum shuleni humo kujadili hatua zitakazofuata.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi, Bi Joylene Cherono na mwenyekiti wa PTA, Bw Richard Chelule, wazazi hao waliamua kuwa hawatahama katika ardhi hiyo.