Sijuti kamwe kukutana na 'Baba' – Catherine Waruguru
Na JAMES MURIMI
MWAKILISHI wa Wanawake Kaunti ya Laikipia, Bi Catherine Waruguru, amesema kwamba hajutii hatua yake kukutana na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.
Bi Waruguru alifanya kikao na Bw Odinga kwenye ofisi yake ya Capitol Hill wiki iliyopita, jijini Nairobi, ambapo alitangaza kwamba atakuwa akishirikiana na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kwa manufaa ya wakazi wa kaunti hiyo.
Ingawa hakueleza moja kwa moja sababu ya kuhama kundi la ‘Tangatanga’ ambalo limekuwa likimfanyia kampeni Dkt William Ruto, mbunge huyo alisema kuwa lengo lake kuu ni kushirikiana na serikali iliyo mamlakani.
“Nitashirikiana na serikali iliyo uongozini kwa sasa,” akaeleza kwenye mahojiano na Taifa Leo bila kurejelea lolote kuhusu kuhusu kundi la ‘Tangatanga.’
Bi Waruguru amekuwa miongoni mwa viongozi ambao hawajakuwa wakisita kumpigia debe Dkt Ruto, hasa katika eneo la Laikipia na ukanda wa Mlima Kenya.
Licha ya hatua hiyo, mbunge huyo, maarufu kama ‘Mama Simba’, alisema kuwa hajali hisia za wakosoaji wake.
“Nafahamu kuwa mwelekeo wangu umezua hisia mseto. Hata hivyo, hilo linatarajiwa kwenye siasa. Nitayakumbatia maoni ya kila mmoja,” akasema.
Tayari, ameeleza kuunga mkono Mpango wa Maridhiano (BBI) unaopigiwa debe na Rais Kenyatta na Bw Odinga.
Bi Waiguru ni miongoni mwa washirika wa Dkt Ruto wanaopangiwa kutolewa kwenye kamati mbalimbali kwenye Bunge la Kitaifa na Jubilee kwa madai ya “kukiuka kanuni za chama.”
“Nafahamu kuhusu ninachofanya. Lazima mtu aangalie mustakabali wake,” akajitetea.
Bi Waruguru huwa anahudumu kama Naibu Mwenyekiti kwenye Kamati ya Bunge Kuhusu Maslahi ya Wabunge.