Soko jipya la Limuru lafunguliwa
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa Limuru wamepata afueni baada ya soko jipya la Limuru kufunguliwa rasmi.
Gavana wa Kaunti ya Kiambu Dkt James Nyoro alizuru soko hilo huku akitoa barakoa kwa wakazi.
Alisema kila mmoja atatafutiwa nafasi ya kuendesha biashara yake bila kubaguliwa.
“Jambo muhimu kwa sasa ni kuhakikisha kila mmoja anajitenga na mwenzake kwa kuweka umbali wa mita moja hivi,” alisema Dkt Nyoro.
Aliwahimiza wafuate sheria zote zilizowekwa na serikali ili kukabiliana vilivyo na homa ya Corona.
“Kwa wakati huu cha muhimu ni kunawa mikono kila Mara na kuhakikisha mnaweka nafasi kwa mwenzako aliye karibu,” alisema gavana huyo.
Aliyasema hayo mnamo Ijumaa,alipozuru soko hiyo ili kujionea mwenyewe jinsi imedumisha usafi unaostahili.
Wakati huo pia aliwapa wanabodaboda barakoa, huku aliwahimiza kuvitumia kila Mara.
Aliwashauri wanabodaboda na Tuk Tuk wafuatevsheria zote bzilizowekwa kwa kubeba watu wachache ili kukabiliana na Corona.
“Ningetaka kuwahimiza mfuate sheria iliyowekwa na serikali ili tupambane na janga hilo la Corona. Kila mmoja anastahili kujihusisha na juhudi hizo ili tufanikiwe,” alisema Dkt Nyoro.
Alisema wiki ijayo atazuru maeneo mengine ili kujionea jinsi mambo yanavyoendeshwa.
Kwa muda wa wiki mbili iliyopita gavana amezuru maeneo mengi katika kaunti hiyo ili kuhakikisha wananchi wanafuata maagizo yote wanayopewa na serikali.
Tayari maeneo mengi ya kaunti hiyo yamewekwa maji kwenye vituo muhimu kama Sokoni, hospitali, vituo vya polisi na hata barabarani
Kwa muda wa wiki moja iliyopita soko zote za kaunti ya Kiambu zilinyunyiziwa dawa ili kuangamiza virusi vya Corona.
Kwa muda wa wiki mbili sasa soko zote za kaunti ya Kiambu zimedumisha usafi baada ya sheria Kali kuweka na kaunti hiyo.
Ilani imetolewa kila mahali kwa yeyote atakayekiuka sheria hizo atachukuliwa hatua za kisheria.