Habari Mseto

Sonko anavyotumia Sh100m kumaliza mbwa jijini

June 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na COLLINS OMULO

SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi imeanzisha zoezi la kumaliza mbwa koko ambao wanazurura ovyo katika wadi 70 za jiji.

Kampeni hiyo ambayo inalenga kumaliza tatizo la wanyama hao ambao wamekuwa wakitatiza shughuli linaingia katika wiki yake ya pili, baada ya kuaznishwa Mei 28.

Hatua hiyo ilifuatia tangazo la serikali ya kaunti hiyo mnamo Aprili kuwa ilikuwa imetenga Sh100 milioni, kuthibiti idadi ya mbwa koko, ambao wanakisiwa kuwa 50,000 na ambao wanasemekana kuhatarisha maisha ya wakazi.

Zoezi hilo ambalo linalenga Kaunti-Ndogo zote 17 za Nairobi litachukua siku 138, huku timu ya serikali hiyo ikilenga kufagia wanyama hao katika maeneo yote.

Kupitia barua iliyoandikwa na mkurugenzi wa udaktari wa mifugo kaunti hiyo Dkt Murithi Muhari, mbwa wote ambao hawamilikiwi na mtu ama wale ambao wanazurura watavamiwa na timu hiyo, huku wale ambao ni hatari watauawa.

Alisema kuwa kwa sasa kaunti hiyo itakumbana na tatizo la mbwa kuzurura ovyo ovyo, ambapo watu wanaumwa, kujeruhiwa na hata kuuawa.

“Sheria ya jiji kuhusu uthibiti na maslahi ya mbwa inasema kuwa watu wote wanaomiliki mbwa Nairobi wanapaswa kuwa na leseni na wawe wakizichukua upya kila mwaka. Aidha, mbwa hao sharti wawe wamedungwa chanjo kwanza. Sababu ya barua hii ni kuomba usafiri (magari mawili spesheli na mawili ya kawaida) na mafuta ya kufanya shughuli hizo,” Dkt Murithi akasema katika barua hiyo ya Mei 13, iliyotumwa kwa mkurugenzi wa masuala ya usimamizi wa jiji.

Barua hiyo ilisema kuwa zoezi hilo lingeanzia eneo la Dagoretti Kaskazini kwa siku 10, kabla ya kuendelea eneo la Dagoretti Kusini kwa siku sita.

Baada ya hapo maafisa wa kazi hiyo wataelekea mtaa wa Westlands kwa siku nane, Embakasi kusini kwa siku sita, Embakasi ya kati kwa siku nane, Embakasi Mashariki kwa siku sita, Embakasi magharibi kwa siku 10 na Embakasi Kaskazini kwa siku nane.