• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Sura mbili za Raila kuhusu masaibu ya Waiguru

Sura mbili za Raila kuhusu masaibu ya Waiguru

Na WAANDISHI WETU

MCHAKATO wa kuamua hatima ya Gavana Anne Waiguru unapoanza leo katika bunge la seneti, macho yote yanaelekezwa kwa kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kujua iwapo atamtetea kinara huyo wa Kaunti ya Kirinyaga au la.

Kwa upande mmoja Bw Raila amekuwa akipinga tetesi kuwa ana mpango wa kumuokoa Bi Waiguru kwa kuwashawishi maseneta wa ODM kuzuia juhudi za kumng’oa gavana huyo huku wabunge wa chama hicho wakiongozwa na Bw Junet Mohamed wakisema ODM itafanya juhudi zote kumwepusha gavana huyo kubanduliwa mamlakani.

Jana, Bw Raila aliruka msimamo wa chama chake kwamba kitamtetea Gavana Waiguru (pichani) dhidi ya kung’olewa mamlakani.

Awali duru zilikuwa zimesema Bw Odinga alikutana na Bi Waiguru wiki iliyopita kujadiliana jinsi atakavyotumia mamlaka yake kumnusuru.

Ijapokuwa Bw Odinga alikanusha ripoti hizo, Bw Junet wikendi alisema ODM imeamua kuwa itamtetea gavana huyo ambaye bunge la kaunti yake lilipitisha hoja ya kumtimua. Lakini, jana Bw Odinga alisisitiza kuwa hajajaribu kuingilia suala hili kushawishi matokeo yake.

“Masenea wafanye kazi waliyopewa na Wakenya, waone haki imetendeka kwa kila Mkenya. Kama mtu atajiokoa mwenyewe ni kulingana na ukweli uliopo,” akasema baada ya kuthibitishwa kutoambukizwa virusi vya corona katika kituo cha afya cha Mbagathi.

Mgawanyiko umeibuka miongoni mwa maseneta kuhusu iwapo hoja hiyo ishughulikiwe kupitia kamati maalum au maseneta wote.

Maseneta wawili ambao walipendekezwa kuwa wanachama ya kamati hiyo ya wanachama 11 jana walikataa mkondo huo wakitaka uamuzi ufanywe na maseneta wote.

Kiranja wa Wengi Irungu Kang’ata alifafanua kuwa maseneta leo wataamua iwapo suala hilo litashughulikiwa kupitia kamati au maseneta wote.

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja na mwenzake wa Kitui Sammy Wambua walisema mfumo huo ambao ulitumiwa kuamua hatima ya aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu utahakikisha haki kwa pande zote.

“Suala hili sasa limechukua mwelekeo wa kisiasa, itakuwa bora iwapo maseneta wote watashirikishwa kuliamua,” akasema Bw Wambua.

Mnamo Ijumaa kamati ya kuratibu shughuli za seneti (SHBC) ilipendekeza majina ya wanachama ambao wataketi katika kamati hiyo.

Wao ni Gideon Moi (Baringo), Beth Mugo (Seneta Maalum), Anwar Oloitiptip (Lamu), Mohamed Mahammud (Mandera), Johnson Sakaja (Nairobi) na Abshiro Halakhe (seneta maalum).

Kwa upande wa upinzani waliopendekezwa ni Moses Kajwang (Homa Bay), Cleophas Malala (Kakamega), Enoch Wambua (Kitui), Beatrice Kwamboka (seneta maalum) na Judith Pareno (seneta maalum).

Baadhi ya wadau katika siasa za Kirinyaga wameteta vikali kuhusu tetesi kwamba kuna juhudi zinazoendelezwa kumwokoa Bi Waiguru visivyo.

Wamesema kuwa baada ya bunge hilo kumng’atua Waiguru Jumanne iliyopita, sasa kuna njama na hila za kumrudisha mamlakani. Aliyekuwa mpinzani wa Waiguru katika kinyang’anyiro cha ugavana 2017, Bi Martha Karua alilaumu upande wa upinzani kwa kushirikiana na serikali kuu katika njama hizo.

“Ni vyema katiba ifuatwe na kuwe na uwajibikaji wa taasisi za kusaidia taifa hili kutawaliwa kwa mujibu wa sheria wala sio kwa mujibu wa urafiki na mapenzi,” akasema.

Naibu Gavana wa Kirinyaga Peter Ndambiri alisema kuwa “kaunti yetu inangojea tu kuona kile kitafanyika na tutakumbatia maamuzi yote ambayo yatawekwa wazi kama matokeo ya mkondo huu wa kung’atuliwa kwa gavana wetu.”

Ripoti za Charles Wasonga, Valentine Obara na Mwangi Muiruri

You can share this post!

Korti yakataa ombi kufukua aliyekufa kwa corona

Kanuni kali kudumishwa ferini hata baada ya virusi

adminleo