Tambua kwa nini sheria ya kudhibiti harambee tayari imeanza kuzua tumbojoto
UTEKELEZAJI wa hatua ya serikali ya kuwapiga marufuku Maafisa wa Serikali na watumishi wa umma kushiriki harambee kama njia ya kukabiliana na ufisadi na utumizi mbaya wa afisi huenda ukakumbana na vikwazo.
Mbunge Maalumu John Mbadi alisema hatua hiyo haitakuwa na manufaa kwani wanasiasa wataanza kutumia washirika kutoa michango yao.
Alitaja pendekezo hilo kuwa la kibaguzi kwani watu ambao hawako katika kundi la maafisa wa Serikali au Watumishi wa Umma na wanaowania viti vya kisiasa watachukua fursa hiyo kuanzisha harambee. katika maeneo bunge wanayolenga.
“Kwa hali ilivyo, kuna mapungufu, kuna ubaguzi. Iwapo ni lazima uweke sheria ya harambee basi iwahusu watu wote. Hebu tuwe na pendekezo kwamba yeyote anayechangia harambee atapigwa marufuku kuajiriwa serikalini au kuwania kiti chochote cha kisiasa kwa miaka mitano,” Bw Mbadi alisema.
Wakati huo huo, wafanyakazi kutoka viwanda vya sukari vinavyomilikiwa na serikali, wamesema Sh654 milioni ambazo zilitolewa wiki jana, hazitoshi kufufua viwanda hivyo ambavyo vinaelekea kuporomoka kutokana na changamoto za kifedha.
Wamelaumu Wizara ya Kilimo kwa kuwapuuza wafanyakazi 8,000 ambao wamewajibika kwa miaka kadhaa bila malipo yoyote. Wiki jana, wakulima wa miwa walinufaika baada ya kulipwa Sh354 milioni huku wafanyakazi nao bado wakiidai serikali Sh5 bilioni.
Katibu katika Wizara ya Kilimo, Kipronoh Ronoh alitoa Sh300 milioni kwa wafanyakazi kwenye viwanda vya Nzoia, Chemelil, Sony, Muhoroni na Shirika linalohusika na utafiti kwenye sekta ya ufugaji na kilimo (KALRO).
Kati ya pesa hizo, Sh150 milioni zitatumika kuwalipa wakulima wa Nzoia huku Sh150 milioni zikielekezwa katika kulipa mishahara ya wafanyakazi Chemelil, Sony, Muhoroni na Kalro kununulia miche ya miwa.
“Inashangaza kuwa wizara imeamua kulipa Nzoia Sh150 milioni kisha kutoa pesa sawa na hizo zigawanywe kwa wafanyakazi wa viwanda vinne. Hili ni jambo ambalo halikubaliki na linatumika kutugawanya,” akasema Katibu wa Muungano wa Wafanyakazi katika Sekta ya Kilimo cha Miwa (KUSPAWO), Bw Francis Wangara.
Katibu huyo alisema hatua hiyo inaenda kinyume na ahadi aliyotoa Rais William Ruto kuwa Sh600 milioni zingetengwa kama malipo kwa wakulima wa viwanda hivyo vinne.
“Kwa mujibu wa mipango, kila kiwanda kingepokea Sh150 milioni,” akaongeza.
Bw Wangara alisema kuwa watakwamisha kukodishwa kwa viwanda vya miwa hadi serikali ilipe madeni hayo.