Habari Mseto

Tanzania yazidi kupaa katika tasnia ya filamu na sinema Kenya ikiendelea ‘kupangapanga tu mambo’

Na WINNIE ONYANDO August 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu, amemtengea ardhi na kumpa nyota wa Hollywood Idris Elba kibali cha kuzindua studio ya filamu nay a kufyatua michezo ya sinema nchini humo.

Haya yanajiri huku Serikali ya Kenya ikiendelea kusuasua katika harakati zake za ‘kupangapanga’ mambo.

Tanzania ambayo ni jirani ya Kenya imepiga hatua hiyo muhimu baada ya majadiliano kati ya Elba na Rais Suluhu mnamo Januari 2023 katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia nchini Uswisi.

Elba, anayesifika kwa uigizaji wake katika filamu za ‘Luther’ na ‘The Wire’, amekuwa na nia ya kuendeleza tasnia ya uigizaji kupia filamu na michezo ya sinema barani Afrika.

Akiwa na asili ya Sierra Leone na Ghana, mwigizaji huyo wa Uingereza anatazamia kuansisha studio ambayo ni ya hadhi ya kushindana na zile za Hollywood, Nollywood na Bollywood.

Waziri wa Uwekezaji wa Zanzibar alisema kwa kutania, “Sina uhakika tutaiitaje Zanzibar sasa, iwe Zollywood au Zawood!”

Msemaji wa Rais alisema hatua hiyo haitafaidi Tanzania pekee bali pia Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.

Kenya kwa upande wake bado inaendelea ‘kupanga panga’ mambo katika juhudi za kutimiza ahadi ya kujenga studio za kisasa katika kila kaunti kama alivyoahidi Rais William Ruto mnamo Agosti 2023.

“Tutashirikiana na serikali za kaunti ili tuweze kutoa fursa kwa kila msanii awe katika shule ya msingi au sekondari kutoa nyimbo zake bila kikwazo chochote,” Rais Ruto alisema alipohudhuria Tamasha za Kitaifa za Muziki (KMF) katika Ikulu ya Nakuru.