Habari MsetoSiasa

Tikiti: ODM sasa yatishia kuadhibu Gavana Obado kwa kupinga chama

July 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

VIVERE NANDIEMO na BARACK ODUOR

MAAFISA wa Chama cha ODM wametishia kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Gavana wa Migori, Bw Okoth Obado, kufuatia hatua yake ya kupinga msimamo wa chama kuhusu uchaguzi mdogo wa useneta katika kaunti hiyo.

Chama hicho Ijumaa kilimkabidhi waziri wa zamani Ochillo Ayacko tikiti moja kwa moja kuwania wadhifa huo uliobaki wazi baada ya kifo cha aliyekuwa seneta Ben Oluoch Okello.

Kulikuwa na wanasiasa wanane waliowasilisha ombi la kutaka tikiti hiyo ya ODM kwa uchaguzi huo mdogo uliopangiwa kufanyika Oktoba 8.

ODM ilitangaza uamuzi wake saa chache baada ya mahakama ya rufaa ya Kisumu kuamua kwamba Bw Obado alishinda ugavana kihalali, kwenye kesi iliyokuwa imewasilishwa na Bw Ayacko kupinga matokeo ya uchaguzi wa ugavana.

Bw Obado aliapa hataunga mkono uamuzi wa ODM kumpa hasimu wake wa kisiasa tikiti moja kwa moja kuwania useneta akataka wakazi wa Migori wasiunge mkono mgombeaji wanayesukumiwa kwa lazima na maafisa walio Nairobi.

Wakizungumza Jumamosi kwenye harambee katika eneo la Suna Magharibi, viongozi wa ODM wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi katika chama hicho Junet Mohamed na Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi, walimkashifu gavana huyo na kudai anasaliti chama.

“Hatutaruhusu kuwe na wasaliti chamani. Haiwezekano kwamba unafurahi unapopewa tikiti ya ODM kuwania wadhifa wa kisiasa lakini unakasirika mwenzako akipewa,” akasema Bw Mohamed ambaye pia ni Mbunge wa Suna Mashariki.

Aliongeza: “Ukipinga ODM Migori, tutakabiliana na wewe vikali. Hakuna vile unashinda kiti uchaguzini kupitia chama hiki kisha unaanza kukimbia huku na kule kukikashifu baadaye. Tutakufunza adabu, wewe subiri tu utaona.”

Hata hivyo, kwenye kikao cha wanahabari siku hiyo hiyo, Bw Obado alikosoa viongozi wanaomkashifu akasema wao hao ndio waliomuunga mkono mgombeaji huru wa ugavana katika uchaguzi uliopita ilhali yeye ndiye alikuwa mgombeaji kwa tikiti ya ODM. Kulingana naye, itakuwa haki kama wanachama wa ODM waliompinga mwaka uliopita wataadhibiwa kwanza.

“Licha ya kuwa nilikuwa na tikiti ya ODM, ni viongozi wao hao ambao walikuwa wakidai nimeasi chama na wakapiga kampeni kunipinga, hakuna aliyewalaumu. Sitakubali kutishwatishwa,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Wandayi alisema viongozi wa chama watashauriana na kuamua hatua ya kinidhamu itakayochukuliwa dhidi ya gavana huyo.

“Mtu mwingine yeyote yuko huru kumpinga Ayacko lakini kama wewe ni mwanachama wa ODM, bila kujali wadhifa wako katika jamii, hatutasita kukuadhibu na utashangaa,” akasema Mbunge huyo wa Ugunja. Mbunge wa Suna Magharibi Peter Masara na Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Migori Pamela Odhiambo, waliomba wanasiasa wa ODM waheshimu chama hicho na kumuunga mkono Bw Ayacko.

“Sote katika ODM lazima tufuate msimamo wa chama katika uchaguzi mdogo ujao. Lazima tuthibitishe uzalendo wetu kwa chama kwa kumuunga mkono Bw Ochillo,” akasema Bi Odhiambo. Kwingineko katika Kaunti ya Homa Bay, dalili zimeonyesha kuwa ODM imeanza kuwashawishi wanasiasa waliokuwa wagombeaji huru katika uchaguzi uliopita warudi chamani.