Tumbojoto kwa matajiri walionyakua ardhi Mombasa karibu na Bahari Hindi
NA MOHAMED AHMED
HALI YA TUMBOJOTO imewashika matajiri katika Kaunti ya Mombasa na kwingineko nchini kwa hofu ya kubomolewa kwa majumba waliyojenga eneo la Bahari Hindi.
Uwezekano wa kubomolewa kwa majumba hayo katika eneo la Kibarani, umetokana na hatua ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kukamilisha uchunguzi wake, ambao kulingana na mwenyekiti Abigail Mbagaya unaonyesha mabwenyenye zaidi ya 25 walinyemelea ardhi ya bahari na kuwekeza katika miradi ya mamilioni ya pesa.
Bi Mbagaya alisema ripoti hiyo itasaidia umma kurudishiwa ardhi hiyo, akisisitiza kuwa bahari haiwezi kumilikiwa na watu binafsi.
“Sitaki kuongea sana kuhusu ripoti hiyo kabla haijapelekwa kwa Rais. Lakini ninataka kusisitiza kuwa hatuwezi kukubali bahari iwe inamilikiwa na watu binafsi. Hilo haliwezekani,” akasema Bi Mbagaya.
Alisema baada ya kukabidhi ripoti hiyo kwa Rais Uhuru Kenyatta katika muda wa wiki mbili zijazo, jukumu la kuamua iwapo majumba yaliyojengwa eneo la bahari yatabomolewa litakuwa la taasisi husika za Serikali ikiwemo NEMA na serikali ya Kaunti ya Mombasa.
“Sisi tutafanya kazi yetu na wale wanaohusika katika awamu hiyo nyingine basi wafanye kazi yao kama inavyotarajiwa,” akaeleza mwenyekiti huyo.
Miongoni mwa miradi iliyoekezwa katika ardhi hiyo iliyoko eneo la Kibarani, Kaunti ya Mombasa ni pamoja na mabohari na maeneo ya kuweka kontena zikisubiri kusafirishwa (CFS).
NLC imekuwa ikichunguza unyakuzi wa ardhi hiyo kwa mwezi mmoja uliopita kufuatia agizo la Rais Kenyatta.
Sasa, mabwenyeye wanaomiliki ardhi hiyo, ambao baadhi ni marafiki wa karibu wa wanasiasa, wameshikwa na wasiwasi kwa kutojua hatima ya miradi yao.
“Ripoti imekamilika na kilichosalia sasa ni kukutana kwa makamishna wa tume ili tujadili ripoti hiyo kabla ya kuipeleka kwa Rais Kenyatta wiki mbili zijazo,” akasema Bi Mbagaya katika mahojiano na Taifa Leo.
Kulingana na wafanyakazi katika kampuni mbili miongoni mwa zilizo katika ardhi hiyo waliiambia Taifa Leo kuwa wasimamizi wa kampuni hizo wapo katika hali ya wasiwasi.
“Hakuna barua zozote ambazo zimetumwa kufikia sasa lakini kuna wasiwasi mkubwa hapa. Wadosi wanahofia kupoteza mali zao,” akasema mdokezi huo.
Mnamo Julai, Rais Kenyatta alielekeza kuwa hati miliki zote za ardhi hiyo zichukuliwe kutoka mikononi mwa mwabwenyenye na ardhi hiyo igeuzwe kuwa bustani kama ilivyoombwa na serikali ya Kaunti ya Mombasa.
Shirika la Reli na la Kenya Meat Commission ni miongoni mwa taasisi zinazomulikwa na NLC.
Aliyekuwa waziri wakati wa serikali ya Rais Mstaafu Daniel Moi, Bw Mohammed Sajjad pia ni miongoni mwa watu binafsi waliolengwa na NLC kwa unyakuzi wa ardhi hiyo. Wengine ni Swaleh Hassan Ali, Halid Ahmed, Esmail Ibrahim, Haji Ahmed Adam, Abdi Elmi Ali, Osman Farah na Anverali Mohamed Sidik.
Kampuni zinajumuisha Ancient Inland Seas, M Tech Building Works, Multiple ICD, Makupa Transit, Talib Bulk Oil Terminal, Wedam Limited, Garissa Holdings Limited, Roosevelt Limited na Mitchel Cotts Kenya Limited.
Zingine ni V. Naram Mulji Properties, Belport Limited, Tiba Freight Forwarders Limited, Civicon Limited, Gapco Kenya Limited, Soko Properties, Mat International Limited na Mat International Terminal.