• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 7:55 PM
Tunataka kukutana na Uhuru –  Kalonzo, Mudavadi na Weta

Tunataka kukutana na Uhuru – Kalonzo, Mudavadi na Weta

CHARLES WASONGA, STEPHEN MUTHINI na WYCLIFFE MUIA

KIONGOZI wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amependekeza mkutano kati ya vinara watatu wa NASA na Rais Uhuru Kenyatta ili kuwepo kwa kile anachokitaja kama muzungunzo yanayojumuisha wote.

Anataka Rais akutane naye pamoja na wenzake Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya).

Akiongea mjini Machakos alipokutana na viongozi wa kidini kutoka Ukambani, Bw Musyoka alisema amekuwa akihimiza kufanyika kwa mazungumzo lakini sharti mazunguzo hayo yashirikishe viongozi wote.

“Tulipokutana na ndugu yetu Raila Odinga mnamo Jumatatu na akatueleza walichojadiliana na rais, tulihisi kuwa tunapaswa kukutana na Uhuru iwapo atakubali. Iwapo hatakubali ni sawa hatuwezi kumlazimisha kukutana nasi,” alisema Bw Musyoka.

“Sisi watatu tungependa kukutana na rais ili tuthibitishe alichomwambia Raila,” akaongeza.

Lakini akiongea baada ya kuhudhuria misa ya wafu ya mwendazake msomi Alloys Tumbo Oeri katika kanisa la Consolata Shrine jijini Nairobi, Bw Wetangula alionekana kutofautiana na Bw Musyoka kuhusu kukutana na Rais Kenyatta.

“Tunapaswa kusahau yale yaliyopita. Tunapaswa kusamehe na kusahau yaliyopita. Sharti tulenge amani na umoja kwa sasa,” alisema Bw Wetangula.

“Bw Odinga, Bw Kalonzo Musyoka, Bw Musalia Mudavadi na mimi ni kama pacha. Tutafanya kazi pamoja kuhakikisha hatuhujumu juhudi hizi za kuunganisha taifa,” akasema Bw Wetang’ula akiongea baadaye katika Bunge la Seneti.

Naye kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale vilevile alipuuzilia mbali wito wa Bw Musyoka akisema mkutano wa Bw Odinga na Rais Kenyatta ulitosha kuanzisha mchakato wa umoja nchini.

“Mkutano wa Rais Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga hapo Machi 9 ulitosha. Vinara hao wengine ambao sasa wanaitisha mkutano na Rais wanafaa kuunga mkono wawili hawa,” akasema Bw Duale.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini alifafanua kuwa mwafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga haulengi kuunda serikali ya muungano bali kuunganisha nchini kwa ajili ya maendeleo.

Bw Duale alisema muungano wa upinzani bado utakuwa ukiendelea kutekeleza wajibu wake wa kupiga msasa utendakazi wa serikali ndani na nje ya bunge na kushirikiana na serikali kutatua changamoto zinazowakabili Wakenya.

Akiwasilisha hoja rasmi, Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini alipongeza ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga akisema utaunganisha taifa na kuimarisha ukuaji wa uchumi.

Bw Mbadi kwa mara ya kwanza alimtambua Kenyatta kama Rais halali.

 

You can share this post!

Mchuano wa Kenya dhidi ya Misri U-20 wafutwa

‘Jicho Pevu’ azua msisimko kwa ufasaha wa lugha bungeni

adminleo