Tutaendelea kupokea pesa za wanasiasa, Askofu aapa
Na NDUNGU GACHANE
ASKOFU wa Kanisa la Kianglikana (ACK) amewashutumu vikali viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakiyakashifu makanisa kwa kupokea fedha zilizopatikana kwa njia ya ufisadi, akisema yataendelea na mtindo huo hadi pale mahakama itakapowapata na hatia viongozi wanaodaiwa hupora pesa kisha kuzitoa kanisani.
Askofu Timothy Gichere wa Dayosisi ya ACK Mlima Kenya ya Kati, alisema hakuna mwanasiasa anayefaa kudai mwenzake anatoa pesa za wizi kwa makanisa ilhali vyombo vya sheria havijampata anayerejelewa na hatia ya kushiriki ufisadi.
Bw Gichere vilevile alisema kanisa halina mbinu ya kutambua iwapo fedha zinazotolewa kwenye michango ya harambee zimeibwa na akawataka wanaokashifu makanisa kuviruhusu vyombo vya sheria kutekeleza wajibu wao badala ya kuingiza siasa kwenye suala hilo.
“Viongozi wanapofika kanisani na kuchangisha fedha, hatuwezi kukataa kwa sababu hatuna njia za kutambua iwapo fedha hizo ni za ufisadi au la. Kanisa haliwezi kuwaita watu wafisadi au waporaji kwa sababu hilo ni jukumu la mahakama.
“Naomba tuache sheria ichukue mkondo wake bila kuingiza siasa ili wafisadi wakamatwe na kufikishwa mahakamani,” akasema Bw Gichere. Askofu huyo aliyekuwa akizungumza katika Gereza la Murang’a alipoongoza Waumini wa ACK kuadhimisha Pasaka na wafungwa, alisema kanisa hilo linaunga mkono vita dhidi ya ufisadi ila akawataka viongozi kukoma kutatiza vita hivyo kwa kuingiza siasa.
Vilevile aliwaonya wanasiasa dhidi ya kutumia majukwaa kanisani kuhubiri chuki na ukabila akisema wanafaa kufika kanisani kupokea mafunzo ya kidini badala ya kushiriki siasa.
“Si vyema kwa wanasiasa kutumia muda wanaopewa kanisani kuhubiri chuki na kufanya kampeni. Wanafaa kuhudhuria ibada ili kulishwa chakula cha kiroho badala ya kutumia muda wao wa kuhutubu kuwashambulia wanasiasa wenzao,” akaongeza Askofu huyo.
Matamshi ya Bw Gichere yanakuja siku chache tu baada ya kinara wa upinzani Raila Odinga kuwashtumu baadhi ya viongozi wa kidini kwa kupokea fedha kutoka kwa wanasiasa waliobobea katika uporaji wa mali ya umma.
Bw Odinga alidai pesa nyingi zinazotolewa makanisani kila wikendi na baadhi ya viongozi hupatikana kwa njia za ufisadi na akataka makanisa kuchunguzwa kwa kutumiwa na wanasiasa kama vituo vikuu vya ulanguzi wa fedha.
“Kuna baadhi ya viongozi wa kidini ambao wanazingatia maadili ya Kristo lakini wengine hawafanyi hivyo. Tunafaa kuuliza kunakotoka mamilioni yanayotolewa makanisani kila wikendi. Inakuaje mtu hulipwa mshahara wa Sh1 milioni ilhali anatoa mchango wa Sh20 milioni kila mwezi?” akauliza Bw Odinga.