Uchawi wa kutengeneza pombe haramu wafichuliwa
Na KNA
MAAFISA wa utawala katika Kaunti Ndogo ya Bondo, Kaunti ya Siaya wamefichua mbinu za kishirikina ambazo watengenezaji pombe haramu wanatumia ili kuepuka kukamatwa.
Wakiongozwa na chifu wa Kata ya Sakwa Kennedy Amollo, maafisa hao walibaini kwamba watengenezaji hao wamekuwa wakitumia ushirikina kuwavutia wateja zaidi na kuepuka kukamatwa.
Kulingana na Bw Amolo, wamefanikiwa kuwakamata washukiwa kadhaa, ambapo walinasa pombe haramu na vifaa wanavyoamini vilikuwa vikitumika kuendeshea ushirikina.
Wanasema wamekuwa wakifanya hivyo kuongeza idadi ya wateja ambao wanawanululia pombe hiyo.
Akiwahutubia wanahabari mjini Bondo, chifu huyo alisema kwamba washukiwa hao wanaamini kwamba ushirikina unaweza kuwalinda dhidi ya kukamatwa na maafisa wa usalama.
Alisema kwamba kwenye operesheni dhidi ya pombe hiyo mnamo Jumapili katika kijiji cha Oseno, walimnasa mshukiwa mmoja akiwa na vifaa hivyo.
Mshukiwa, aliyetambuliwa kama Lizzie Anyango, alipatikana na pombe aina ya Simba Waragi, ambayo imeorodheshwa kuwa haramu.
Walionya kuwa pombe hizo zinahatarisha maisha ya vijana.
Mwezi uliopita,lita 1,000 za muna, bidhaa inayotumika kutengeneza pombe haramu ilipatikana zikiwa imefichwa eneo la Kambakia, Kaunti ya Meru.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya operesheni hiyo, chifu, Bi Mercy Murithi alisema kuwa wamekamata lita 40 za pombe haramu na lita 1,000 za muna, ambayo ilikuwa imefichwa katika maboma ya watu mawili.