Uhalifu waongezeka wakati wa kafyu
Na ONYANGO K’ONYANGO
VISA vya uhalifu vinazidi kuongezeka kwenye kaunti zinazopatikana Kaskazini mwa Bonde la Ufa hasa usiku wakati wa kafyu iliyowekwa na serikali juma moja lililopita kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona.
Wakazi wa magatuzi hayo sasa wanaishi kwa hofu baada ya kuvamiwa na wahalifu waliojihami vikali kwa silaha hatari.
Mnamo Jumatano usiku, mwanamke mmoja alibakwa kisha kuuawa kikatili katika mtaa wa Langas jijini Eldoret na polisi bado wanaendelea kuwasaka wahalifu waliohusika.
Wizi wa kimabavu pia umeongezeka hasa siku mbili zilizopita wahalifu wakifuatilia mienendo ya maafisa wa usalama wanaopiga doria kuhakikisha raia wanazingatia kafyu.
Maduka ya wafanyabiashara yamevamiwa huku nyumba pia zikivamiwa na watu kuibiwa mali yao.
Jijini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, mfanyabiashara Stanley Migaine anaendelea kukadiria hasara ya Sh100,000 baada ya wezi kuvunja na kupora bidhaa zilizokuwa kwenye duka lake Jumanne usiku.
Pia walimwibia fedha ambazo alikuwa amewacha dukani humo.
“Nimeshangaa kwamba wakati wa kafyu, wahalifu hutawala na kupora mali ya wafanyabiashara bila hofu yoyote. Walivunja duka langu usiku na kuhepa na kreti 14 za soda, kadi za mjazo wa simu na Sh16,000 pesa takwimu. Pia walihepa na runinga yangu na bidhaa nyinginezo,” akasema Bw Migaine.
Naibu Kaunti Kamishina wa Turbo Mohammed Mwabudzo ambaye alimtembelea Bw Migaine, aliwaonya wahalifu hao kwamba watanyakwa na kuadhibiwa vikali kisheria huku akitoa wito kwa raia kushirikiana na polisi kuwatambua wahalifu hao wanaotumia kafyu kuwapora.
“Tutazidisha doria ili kuwatokomeza wahalifu na pia tumewaruhusu wawe na walinzi wao wa kibinafsi kulinda biashara zao nyakati za usiku,” akasema.
Wakati huohuo, wakazi wa mitaa ya Kaplombe, Huruma na West Indies pia wamelalamikia kuibiwa na kunyanyaswa na wahalifu nyakati za usiku.
Wakazi hao sasa wanashuku wahalifu hao wanashirikiana na polisi kuwaibia wakati wa kafyu. Wengine nao wanadai kwamba wahalifu hao hufuatilia mahali polisi wapo kisha kutekeleza wizi eneo jingine.
“Wahalifu hao sasa wanashiriki mchezo wa paka na panya na polisi na huvunja maduka na makazi ya watu wakijua kwamba polisi hawako karibu,” akasema mkazi kwa jina John Maina mtaani Huruma.
Mtaani Langas ambako wakazi walilalamikia hali ngumu ya maisha majuzi, mwili wa mwanamke aliyebakwa ulipatikana kwenye mtaro katika eneo la Langas-Kona.? Mkuu wa Polisi Eldoret Kusini jana alisema wanaendelea kuchunguza kisa hicho.
Kamanda wa polisi wa Uasin Gishu Johnstone Ipara naye alisema kwamba polisi sasa watakuwa ange kulinda biashara na mali ya wakazi na pia kuwanyaka wahalifu hao.
Kamishina wa Uasin Gishu Abdirazak Jaldesa naye alisema raia wanaokiuka kafyu na wahalifu watakamatwa .