Habari MsetoSiasa

Uhuru sasa aililia China ilegeze masharti ya madeni

June 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Valentine Obara na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta ameiomba Serikali ya China kulegeza masharti ya madeni ambayo taifa hilo linadai Kenya na nchi nyingine nyingi za Afrika.

Akizungumza katika kongamano la kipekee kati ya viongozi wa Afrika na China, ambalo liliandaliwa kwa njia ya kimitandao usiku wa kuamkia jana, Rais Kenyatta alimwambia mwenzake wa China, Xi Jinping kwamba uchumi umezorota sana Afrika kwa sasa.

Hali hii mbaya ya uchumi imesababishwa na janga la corona ambalo limefanya shughuli muhimu za kibiashara kukwama kimataifa.

“Kwa kuzingatia athari za kiuchumi barani, ningependa kuihimiza China kuongeza zaidi hatua za kulegeza masharti ya madeni na yale ya kibiashara. Hii itayapa mataifa ya Afrika nafasi ya kujikwamua kwa ufufuzi wa kiuchumi,” akasema Rais Kenyatta.

Kongamano hilo lililofanyika kwa njia ya video liliandaliwa na China, Afrika Kusini na Senegal.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ndiye Mwenyekiti wa Muungano wa Afrika (AU) huku Rais wa Senegal Macky Sall akiwa ndiye Mwenyekiti Mwenza wa Shirikisho la Ushirikiano wa Afrika na China (FOCAC).

Katika hotuba yake, Rais Xi aliahidi kwamba serikali yake itaendelea kusaidia mataifa ya Afrika kupambana na janga la corona.

Alimsifu Rais Kenyatta kwa kuhakikisha shughuli hazijakwama katika bandari ya Mombasa na hivyo basi kusaidia katika usafirishaji wa bidhaa licha ya vikwazo vingi vilivyosababishwa na janga la corona.