Habari MsetoSiasa

Viongozi Bondeni wataka Ruto aheshimiwe

March 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na EVANS KIPKURA

MIITO ya kumtaka Naibu wa Rais William Ruto aheshimiwe na kulipwa kwa fidia wakazi waliohamishwa ili kupisha ujenzi wa mabwawa ya Kimwarer na Arror ndizo ajenda kuu zilizotawala mkutanao wa mashauriano kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI) uliofanyika katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet wikendi.

Viongozi na wakazi waliozungumza katika mkutano huo uliofanyika Iten walisema kuwa sehemu mapendekezo yaliyo katika ripoti ya BBI yamezingatia maslahi yao.

Wakiongozwa na Gavana Alex Tolgos, ambaye pia ni mwenyekiti wa BBI katika eneo la Bonde la Ufa, viongozi hao waliorodhesha masuala ambayo wanataka yajumuishwe katika ripoti ya BBI.

“Mengi ya mambo ambayo tulitaka yaangaziwe tayari yamejumuishwa katika ripoti ya BBI,” akasema Gavana Tolgos.

Gavana huyo alisema kuwa wanatumai ripoti ya BBI itasaidi kushughulikia mizozo kuhusu ardhi na mipaka inayoandama kaunti hiyo.

“Ikiwa ripoti hiyo itatekelezwa kikamilifu, Bonde ka Kerio litajumuishwa miongoni mwa maeneo kame (ASAL),” akasema.

Alisema kuwa mapendekezo yaliyopitishwa katika mkutano huo yatakabidhiwa kwa jopokazi la BBI moja kwa moja.

Viongozi wengine waliokuwepo walitilia shaka utekelezwaji wa ripoti hiyo.

“Tumekuwa na majopo mengi ambayo yametoa ripoti kama vile ripoti ya Kreigler, Ndung’u na hata Katiba ya 2010 hazijatekelezwa kikamilifu,” akasema mbunge wa Keiyo David Rono.

Bw Rono alisema kuwa mpango wa BBI umetekwa nyara na baadhi ya wanasiasa wanaojitakia makuu. Mbunge huyo alisema mikutano ya kupigia debe ripoti ya BBI imegeuzwa kuwa majukwaa ya kumshambulia Naibu wa Rais William Ruto.

“Hatuwezi kujifanya kwamba tunaunganisha Wakenya kupitia BBI ilhali kwa upande mwingine tunaendeleza migawanyiko,” akasema Bw Rono.

Suala la kuhusu mapendekezo ya kutaka idadi ya maeneobunge kupunguzwa pia lilijadiliwa kwa kina.

“Kaunti hii ina maeneobunge manne na yamekuwepo tangu Kenya kujipatia uhuru. Hatutaki yaunganishwe au yagawanywe. Tuna idadi ya kutosha watu,” akasema mbunge wa Keiyo Kaskazini James Murgor. Murgor alitaka serikali ifadhili wakulima katika kaunti hizo ili kuboresha uzalishaji wa mazao.

Alisema hakuna haja ya kaunti hiyo kurejelewa kama ghala la chakula ilhali wakulima wanahangaika.

Mwakilishi wa Kike Jane Kiptoo alisema jopokazi la BBI linafaa kuhakikisha kuwa vituo vya kunusuru waathiriwa wa dhuluma za kijinsia vinajengwa katika kila kaunti kote nchini.