Viongozi wa Magharibi waitetea IEBC
BRIAN OJAMAA na BENSON MATHEKA
KIONGOZI wa Ford Kenya Moses Wetang’ula ameongoza viongozi wa magharibi mwa Kenya kushutumu wanasiasa wanaotaka mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati, ajiuzulu.
Akizungumza katika Kanisa Katoliki la Kimaeti katika Kaunti ya Bungoma, Bw Wetang’ula alisema wanasiasa hawafai kuteua maafisa watakaosimamia uchaguzi.
“Mwanasiasa ambaye ana hakika atawania kiti katika uchaguzi mkuu ujao hafai kujiamulia nani atakuwa refarii (mwenyekiti wa IEBC),” akasema.
Bw Wetang’ula alihoji kwamba serikali inastahili kumpa Bw Chebukati rasilimali za kutosha kuendesha kura ya maamuzi ya Mpango wa Maridhiano (BBI) badala ya kumtaka ajiuzulu.
“Mpe muda wa kutosha Bw Chebukati kujitayarisha kwa ajili ya kura ya maamuzi, endapo mswada wa BBI utaidhinishwa na mabunge ya kaunti. Chebukati pia anajiandaa kwa ajili ya chaguzi ndogo katika maeneobunge ya Kabuchai, Matungu, na kaunti za Machakos na Nairobi,” akaeleza kiongozi huyo ambaye pia ni Seneta wa Bungoma.
Bw Wetang’ula alisema Bw Chebukati anastahili kuungwa mkono wakati huu mbapo IEBC inajiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.Kauli hiyo iliungwa mkono na viongozi wengine kutoka eneo la Magharibi, wakimshutumu kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kutaka Bw Chebukati atimuliwe.
Wabunge hao wakiongozwa na Chris Wamalwa (Kiminini) na Didmus Barasa (Kimilili) walimtaka Bw Odinga kukoma kuingilia majukumu ya mwenyekiti wa IEBC.Walikuwa wakizungumza wikendi katika mazishi ya mbunge wa Kabuchai, James Lusweti, katika Kaunti ya Bungoma.
Viongozi hao walisema kuwa Bw Odinga hana mamlaka ya kushinikiza IEBC kuendesha shughuli zake anavyotaka yeye.“Bw Odinga si mtumishi wa serikali na wala hana mamlaka ya kumtimua yeyote.
Makamishna wa IEBC wanafanya kazi nzuri na hawafai kuhangaishwa na wanasiasa. IEBC ni tume huru ambayo haifai kufuata maelekezo ya mtu yeyote kutekeleza majukumu yake,” akasema Bw Barasa.
Mbunge huyo aliapa kuongoza kampeni ya kupinga mswada wa BBI kuhakikisha unakataliwa na Wakenya.“Mswada wa BBI hauna lolote la kusaidia Wakenya; unalenga kunufaisha wachache,” alihoji.
Bw Odinga wiki iliyopita alishambulia IEBC kwa kutaka kutengewa kiasi kikubwa cha fedha kukagua saini zinazounga mkono mswada wa BBI.
Kigogo huyo wa ODM, ambaye amekuwa mstari wa mbele kupigia debe BBI, alitaka Bw Chebukati kujiuzulu ikiwa amelemewa na kazi.
Kulingana na waziri mkuu huyo wa zamani, Bw Chebukati na makamishina wenzake katika IEBC walikuwa wakichelewesha mchakato huo.
“Ikiwa hawataki kufanya kazi wanastahili kuondoka ili Wakenya wengine waliohitimu wafanye kazi hiyo,” Bw Odinga akasisitiza.
Alisema hayo baada ya IEBC kueleza kuwa inahitaji Sh241 milioni kukagua saini hizo.Tayari Wizara ya Fedha imetoa Sh93.7 milioni kwa ajili ya kukagua saini za BBI.
Bw Wetangula alisema kuwa mtu anayemezea mate kiti cha uchaguzi hawezi kuamua au kumuagiza refarii jinsi ya kuendesha uchaguzi huo.