Viongozi wa Mulembe wajipanga kuchukua kiti cha Gachagua endapo atatemwa
BAADHI ya wabunge wa eneo la Magharibi wameanza kampeni kumpigia debe Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kukalia kiti cha naibu rais iwapo Bw Rigathi Gachagua atatimuliwa.
Mbunge wa Khwisero Christopher Aseka na mwenzake wa Matungu Peter Nabulindo wanaongoza kikosi cha kumuondoa afisini Bw Gachagua kwa faida ya Bw Mudavadi.
Wabunge hawa wanamsawiri Bw Mudavadi kuwa kiongozi mtulivu asiyezua rabsha.
Kulingana na Bw Aseka, mkuu wa mawaziri (Musalia Mudavadi) ni watatu katika ngazi ya uongozi serikalini; kwa hivyo, wanaamini, anafaa kuwa naibu rais kiti hicho kitakapokuwa wazi.
“Kulingana na utaratibu wa uongozi, iwapo rais ataondoka ofisini, kiti chake huchukuliwa na naibu rais papo hapo. Kufuata utaratibu huu, endapo naibu rais anaondoka, mkuu wa mawaziri achukue wadhifa huo,” alisema Bw Aseka.
Kwa moto uo huo, Bw Nabulindo alitilia shaka uwezo wa kiongozi kutoka eneo la Mlima Kenya (Gachagua) kukalia kiti cha naibu rais akiendelea kumpigia debe Bw Mudavadi.
“Amewahi kuwa makamu rais na kuwa kiongozi wa ngazi ya juu serikalini. Hata aliwahi kuwa naibu waziri mkuu. Hakuna kiongozi nchini ana hadhi kama hii. Kwa hivyo, Bw Mudavadi anafaa kuteuliwa kuwa naibu rais,” alisema.
Kadhalika, Mbunge wa Lurambi Titus Khamala aliendeleza wimbi la kutetea ufaafu wa viongozi wa Magharibi kurithi wadhifa huo.
“Iwapo nafasi hii itakuja kwa jamii ya Waluhya, hatutakataa. Tutaichukua kwa furaha tukijipanga kwa uchaguzi mkuu wa 2032,” alisema Bw Khamala.
Savula apinga
Lakini Naibu Gavana wa Kakamega Ayub Savula ameshikilia kuwa wadhifu huo ni wa viongozi wa eneo la Kati na unafaa kurejeshwa eneo la Mlima Kenya.
“Sisi kama Waluhya tumetosheka na kiti cha mkuu wa mawaziri kilichotunukiwa Bw Mudavadi, kile cha Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, na nyadhifa za baraza la mawaziri kwa Wycliffe Oparanya na Debora Mulongo pamoja na viti vya wakuu wa mashirika ya serikali. Tunalenga mwaka wa 2032 wakati tutasimama na kiongozi wa Kiluhya,” Bw Savula alisema.
Kisha aliongeza: “Tutatoa tangazo kubwa kama viongozi wa Magharibi na hatuna haja na kiti hicho. Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ndiye kiongozi bora zaidi kuchukua nafasi ya Bw Gachagua iwapo atatimuliwa.”
Hata hivyo, Bw Khamala alisema ni serikali ya Kenya Kwanza na Rais William Ruto wana mamlaka ya kuchagua atakayekuwa naibu rais kama Bw Gachagua atapigwa teke.
Naye Bw Savula ameungama kuwa Rais William Ruto huenda akashindwa kumuokoa naibu wake hata kama ataamua kumlinda.
“Hata kama rais ataongea na wabunge wamwache Gachagua aendelee na kazi, sidhani kama atafaulu kwa sababu naibu rais hawaheshimu wabunge,” alisema.