Habari Mseto

Vioski vya muguka vyaanza kubomolewa Mombasa

August 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

SIKU moja baada ya wawakilishi wa wadi ya Mombasa kuanzisha mikakati ya kupiga marufuku uuzaji wa muguka askari wa kaunti Jumatatu walianza kubomoa vibanda vinavyouza mmea huo.

Zaidi ya askari 20 walivivamia vibanda hivyo na kuvibomoa eneo la Tononoka ambapo soko kubwa la Muguka hupatikana.

Kamati ya Afya ya bunge la Mombasa ilisema kuwa Muguka umeathiri pakubwa ndoa nyingi na kuchangia kuvunjika kwa baadhi ya ndoa hizo.

Naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Fatma Kushe alisema kuwa idadi kubwa ya vijana wanaotumia mmea huo inatishia kizazi kijacho.

Jumatatu, mkurugenzi wa askari wa kaunti Mohammed Amir alisema kuwa ubomozi huo ulifanyika baada ya agizo kutoka katika kitengo cha afya kufuatia ongezeko la visa vya vijana wadogo kuingia katika uraibu huo.

Ubomoaji huo pia unakuja wiki moja baada ya wawakilishi wa wodi ya Mombasa kupendekeza agizo la kupiga marufuku ya Muguka katika kaunti hiyo.

Askari wa kaunti ya Mombasa wang’oa paa la kioski cha muguka eneo la Tononoka Agosti 6, 2018. Picha/ NMG

Hata hivyo kufikia sasa bado serikali ya kaunti haijapitisha agizo hilo la kuzia kuuzwa na utumizi wa Muguka. Mombasa ni kaunti ya tatu sasa ambayo imeingia katika kampeni ya kupiga marufuku mmea huo huku serikali ya Kwale ikiwa tayari imepitisha agizo la kuzuai kuuzwa na kutumiwa kwa Muguka.

Vijana wengi kutoka kwale hununua bidhaa hiyo eneo la Likoni ambapo ni karibu na kaunti hiyo. Kaunti ya Kilifi pia inaendesha mipango ya kuzuia utumizi wa Muguka huku baadhi ya viongozi wakilia ongezeko la matumizi yake miongoni mwa vijana wa shule.

Aidha, jana wafanyabiashara jijini Mombasa walilalamika kuvunjiwa vibanda vyao na kuwashutumu askari hao kutekeleza ubomoaji huo.

“Hakuna agizo lolote ambalo limepitishwa, mbona watuvunjie vibanda vyetu? Sisi kila siku tunalipa ada ya kufanya biashara kwa askari hao wa kaunti leo hii wanatukatizia riziki yetu bila sababu yoyote. Wanataka twende wapi? Ama wanafurahia kukiwa na uhalifu?” akalalama Bw Gabriel Kithaka, ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara eneo hilo la Tononoka.

Mfanyabiashara mwengine Bi Miriam Wangeci, alipinga madai kuwa mmea huo unachangia katika kuvunja ndoa.

“Hayo ni madai tu kama mtu hawezi shughuli basi ni Mungu amemuumba hivyo na sio Muguka.Kuna watu wanatumia dawa za kulevya ambazo wanajua ni mbaya kwa afya lakini bado wanaendelea na shughuli zao kama kawaida,” akasema.