Waandamana wakitaka polisi wasake miili ya waliokufa maji
Na GEORGE SAYAGIE
SHUGHULI za kibiashara mjini Narok zilitatizwa Jumamosi asubuhi baada ya wakazi kuandamana na kufunga barabara ya Narok-Maimahiu wakilalamikia uzembe wa polisi kutotoa miili ya wanaume wawili waliokufa maji wakijaribu kumwokoa mwanafunzi aliyekuwa anasombwa na maji katika mto uliovunja kingo zake Ijumaa usiku.
Waandamanaji walitumia mawe na vikingi vya miti ya stima kufunga barabara hiyo karibu na jengo la bodi ya nafaka na mazao NCPB.
Wakazi hawa waliokuwa na hasira kali walitisha kusitisha shughuli zote hadi pale miili hiyo itakapotolewa.
“Hatutatulia hadi miili hii ipatikane na itolewe kwenye mto huu. Wahasiriwa walisombwa na maji saa 18 yaliyopita na hakuna ishara kutoka kwa polisi ya kushughulikia maiti hao,” mlalamishi mmoja Bw Joseph Salau alisema.
Wenye magari pamoja na watalii waliokuwa wanaelekea katika hifadhi maarufu ya wanyama wa pori ya Maasai Mara walikwama kwenye barabara hiyo kwa zaidi ya saa tatu baada ya barabara kufungwa.
Vurugu zilitanda huku polisi wakiwakabili waandamanaji kwa kuwatupia hewa ya kutoa machozi lakini wananchi wenye ghadhabu waliwashambulia polisi kwa mawe.
Polisi wakiongozwa na Bw Lawrence Opiyo walijisatiti na kuwatuliza waandamanaji.
“Kuna watu wagonjwa kwenye magari , kuna watalii wanaoenda Nairobi kuabiri ndege warudi makwao. Tafadhali fungueni barabara huku tukiendelea kusaka miili ya wanaume hao,” Bw Owino aliwasihi wakazi hao lakini “ hawakumjibu.”
Hatimaye wakazi hao walijitwika jukumu la kusaka miili hiyo na kujitosa katika kidimbwi kimoja kilichoko kwenye mto Kakaya unaovunja kingo zake inaponyesha na kusababisha madhara makubwa.
Maiti za Ntoika Partoip na Moseka Simat ziliondolewa na ndugu yao Bw Dickson Partoip aliambia wanahabari kwamba maafa yaliwakumba wawili hao wakirudi nyumbani kutoka kwa nyanya yao katika kijiji cha Lemanet walikopeleka ng’ombe wawili kuchinjwa wakati wa mazishi yake jana.