Habari MsetoSiasa

Wabunge wa Magharibi watisha kuhama Jubilee baada ya Echesa kutiwa adabu

March 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na SHABAN MAKOKHA

Wabunge wa Jubilee eneo la Magharibi wametisha kuhama chama hicho kulalamikia kufutwa kazi kwa aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa. Hata hivyo, akiongea Jumamosi siku moja baada ya kufutwa kazi, Bw Echesa alisema alipokea habari za kufutwa kwake kupitia vyombo vya habari na kuwataka wafuasi wake kuwa watulivu.

“Rais ana sababu zilizochangia uamuzi wake wa kunifuta,” Bw Echesa aliwaambia waombolezaji katika mazishi ya Henry Tanga Busolo katika kijiji cha Marinda, eneo bunge la Matungu.

“Mimi siye waziri wa kwanza au wa mwisho kufutwa kazi. Nimejiunga na orodha ndefu ya mawaziri ambao wamefutwa kazi lakini hii sio mwisho wa maisha,” akaeleza.

Wabunge Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Didmus Barasa (Kimilili), Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Benard Shinali (Ikolomani) walidai kuwa eneo hilo lilichangia pakubwa kukubaliwa kwa chama cha Jubilee wakati wa marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, 2017 uliosusiwa na watu kutoka Nyanza.

Walilalamika kwamba utawala wa Rais Kenyatta ulianza kulitenga eneo hilo baada ya kuweka muafaka kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Wakiongea katika maeneo tofauti viongozi hao walisema inakera kuwa Rais ambaye anahudumu muhula wake wa mwisho anaonekana kuthamini zaidi eneo la Nyanza kuliko eneo la Magharibi ambalo lilisimama naye katika uchaguzi mkuu wa 2017.

“Ikiwa watu wa magharibi wangekataa kushiriki marudio ya uchaguzi wa urais mnamo Oktoba 26, 2017 walivyofanya watu wa Nyanza, serikali ya Jubilee ingepoteza uhalali wa kuendelea kuwa mamlakani,” akasema Bw Washiali.

Bw Washiali ambaye ni kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa alisema viongozi kutoka eneo hilo wamekerwa zaidi na kufutwa kazi kwa Bw Echesa. Alisema Bw Echesa ni mmoja wa viongozi waliojitolea mhanga kuvumisha Jubilee na Rais Kenyatta katika eneo hilo ambalo limekuwa ngome ya upinzani.

“Echesa aliifanyia kazi Jubilee kwa uaminifu hadi akapoteza kiti cha ubunge cha Mumias Magharibi kwa mgombeaji wa ODM,” akaeleza Bw Washiali.