Wabunge wa Wiper waliounga hoja ya kumtimua Gachagua kuadhibiwa, Kalonzo atangaza
KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amekosa mchakato unaoendelea wa kumfurusha Naibu Rais Rigathi Gachagua akisema wale wa Wiper waliounga hoja hiyo wataadhibiwa.
Bw Musyoka aliwakosoa wabunge 282 waliounga mkono mswada huo uliowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse. Alisema wale wa Wiper ambao waliunga hoja hiyo lazima wafike mbele ya kamati ya nidhamu chamani na kueleza kwa nini walikiuka maagizo ya kutounga hoja hiyo.
“Serikali kwa hakika imeshika mateka bunge. Kama hilo halikuwa wazi hapo mbeleni, matukio ya kutimuliwa kwa Bw Gachagua yalithibitisha. Wabunge wa Wiper waliounga hoja hiyo wajiandae kukabiliwa na adhabu ya chama,” akasema.
Makamu huyo wa rais wa zamani aliandamana na kiongozi wa chama Democratic Action Party-Kenya, Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, Gavana wa zamani wa Kiambu na wanasiasa kadhaa wa Wiper kule Mlolongo alipoyatoa madai hayo.
Bw Musyoka alisema kuwa hana imani na wabunge na maseneta, korti ni kati za asasi ambazo zimetekwa na serikali.
Pia alimhusisha Kinara wa Azimio Raila Odinga kwenye mikataba ya mamilioni baina ya serikali na shirika la India. Alisema mikataba hiyo inayohusu sekta za nishati, huduma ya afya na usafiri, ni kiumbe cha serikali pana inayojumuisha serikali ya Kenya Kwanza na wandani wa Bw Odinga.
Matamshi ya Bw Musyoka yamejiri huku Waziri wa Nishati, Opiyo Wandayi, mwandani wa Bw Odinga akifichua kuwa serikali ilitia saini mkataba wa Sh95 bilioni na Adani Energy Solutions kuimarisha usambazaji wa umeme.
Kampuni hiyo ya India inashiriki mazungumzo na serikali kuhusu kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Inasemekana kuwa kampuni hiyo ya India imetia saini mkataba na serikali kuendesha ajenda ya mpango wa afya kwa wote.