Habari Mseto

Wachapishaji sasa wajitenga na makosa vitabuni

October 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PETER MBURU

WACHAPISHAJI wa vitabu, kupitia muungano wao wa KPA, Alhamisi walijitetea kutokana na malalamishi kutoka kwa umma kuhusiana na baadhi ya vitabu ambavyo vimekosolewa kwa kutoa mafunzo yenye utata.

Maafisa hao wa KPA walitetea baadhi ya mafunzo wakisema yanafaa kwa watoto, huku wakikanusha mengine ambayo yameibua ukosoaji mkubwa kutoka kwa umma kuwa hayakuchapishwa nchini.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa muungano huo, Lawrence Njagi wakati wa kikao na wanahabari jijini Nairobi, maafisa hao waliwataka Wakenya kutofasiri mafunzo ya watoto ‘ki utu uzima’ kwa kuwa wanapotosha maana inayolengwa.

Bw Njagi alitetea ukurasa katika kitabu cha daraja la chini ambao umewaonyesha walimu na wanafunzi wakishangilia ndege ya mwanasiasa, huku akifasiriwa kuwa na mali nyingi na kuishi maisha bora, kuwa unatoa ujumbe wa kuwatia motisha watoto.

Alisema ni watu wazima wanaopotosha ujumbe wa funzo hilo, lakini kwa watoto ni ujumbe wenye umuhimu.

“Hakuna kitu kibaya na ujumbe huo, unafaa kuangaliwa kwa macho ya mtoto, ila si ya mwanasiasa wala sisi watu wazima,” akasema Bw Njagi.

Katika sehemu nyingine ambayo mwanafunzi ameonyeshwa akilima wakati wenzake wakiwa darasani, mwenyekiti huyo wa wachapishaji alisema hiyo ililenga kutoa funzo kwa watoto kuhusu dhuluma zisizofaa.

Lakini muungano huo ulijitenga na vitabu viwili ambavyo vimekosolewa pakubwa, kimoja kikisema matumizi ya kichwa ni kubeba mizigo na kingine kikifundisha watoto mambo yasiyofaa, kuhusu ngono.

“Hiki si kitabu cha Kenya na hakitumiki katika mtaala wetu. Kitabu chenyewe ni cha kutoka Ghana, Afrika Magharibi na hakihusiani kwa vyovyote na wachapishaji wetu.

Nakubaliana kuwa ni makosa, matumizi ya kichwa cha Mwafrika wa kawaida sio kubeba mizigo, kichwa kina matumizi mengi bora,” akasema.

Maafisa hao walijitetea kuwa hawana uwezo wa kuzuia vitabu vinavyonunuliwa kutoka nje ya nchi, wakisema ni jukumu la mzazi kuhakikisha kitabu anachotumia mwanawe kimeidhinishwa na Taasisi ya Kitaifa ya Kukuza Mitaala (KICD).

Walisema vitabu vyote vilivyochapishwa ili kutumiwa kwa mtaala mpya utakaoanzishwa mwaka ujao havina doa, wakisisitiza kuwa vina ubora wa asilimia 100.

“Kabla ya kuruhusiwa na KICD, vitabu hivyo vilifikisha kiwango cha ubora cha asilimia 95 kisha Taasisi hiyo ikapendekeza tunapofaa kurekebisha. Hadi tunavyoongea sasa, vitabu vyote vilivyoko sokoni havina kosa hata kidogo,” akasema Bw Njagi.

Maafisa hao aidha, waliteta kuwa sehemu tata ambazo umma umekosoa hazihusiani kwa vyovyote na mtaala mpya wa elimu, wakisisitiza kuwa mtaala huo ambao unatarajiwa kuanzishwa rasmi Januari unalenga kuhusisha mtoto katika masomo, kwa kumfanya kufikiria kwa kina na kusoma kwa kujifanyia mambo ili kuelewa zaidi.

Walisema japo vitabu vingi walivyochapisha vimejaribu kadri ya uwezo kutoa mafunzo kimaadili inavyostahili, baadhi ya watu wanavikosoa hata mahali ambapo hakuna makosa.

“Baadhi ya mambo yanayosemwa kuwa makosa sio makosa wala ni maoni ya watu ama wanavyodhani watu tu. Kwa watoto mafunzo haya yako sawa,” akasema Bw Njagi.